Na John Buluku, Dar es Salaam
Mojawapo ya mambo yanayopaswa kupewa nafasi katika mjadala wa kisiasa ni uwezo wa kusikiliza na kuchambua hoja kabla ya kuzikubali au kuzikataa. Hili limejitokeza wazi mitandaoni kufuatia mahojiano ya Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk. Asha-Rose Migiro, na mwandishi wa habari Salim Kikeke ambapo alizungumzia matukio ya Oktoba 29, msimamo wa CCM kuhusu ripoti ya tume ya uchunguzi pamoja na hatua zilizochukuliwa na serikali kurejesha amani na utulivu nchini.
Ni muhimu kutambua kwamba Dk. Migiro alikuwa akizungumza kama Katibu Mkuu wa CCM, chama tawala ambacho pia kinaongoza serikali. Kwa nafasi hiyo, alikuwa na wajibu wa kueleza mtazamo wa chama chake kuhusu matukio hayo, namna yalivyotazamwa na hatua zilizochukuliwa baada ya tukio hilo. Hivyo, kwa mtu yeyote anayefuatilia siasa kwa ukaribu, ilikuwa wazi kwamba majibu yake yangebeba mtazamo wa taasisi anayoiongoza na si mtazamo binafsi.
Katika mahojiano hayo, moja ya hoja zilizovuta hisia za wengi ni uamuzi wa CCM kuvipongeza vyombo vya ulinzi na usalama baada ya matukio ya Oktoba 29. Wapo walioona pongezi hizo hazikuwa sahihi, lakini ukifuatilia kwa makini maelezo ya Migiro utaona kwamba hakudai kila jambo lililofanyika lilikuwa kamilifu au lisilo na kasoro. Badala yake, alikiri wazi kuwa dosari zinaweza kuwa zilijitokeza wakati wa utekelezaji wa majukumu yao. Hoja yake kuu ilikuwa kwamba pamoja na changamoto hizo, vyombo vya dola vilifanikiwa kuzuia hali ambayo ingeweza kuisukuma nchi katika machafuko makubwa zaidi.
Hii ni hoja ambayo inaweza kukubaliwa au kupingwa kisiasa, lakini ni hoja inayostahili kujibiwa kwa hoja nyingine badala ya kushambulia mtoa hoja. Katika nchi nyingi duniani, tathmini ya kazi za vyombo vya usalama wakati wa migogoro huwa inaangalia si tu madhara yaliyotokea, bali pia madhara ambayo yangeweza kutokea kama hatua za haraka zisingechukuliwa. Huo ndio msingi wa hoja ambayo Migiro aliijenga katika mahojiano yake.
Jambo jingine muhimu ambalo halipaswi kupuuzwa ni namna alivyopokea matokeo ya tume ya uchunguzi. Badala ya kukataa au kupinga takwimu zilizotolewa, alisisitiza kuwa CCM imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya zaidi ya watu 500 waliopoteza maisha. Alikwenda mbali zaidi kwa kusema kuwa hata kifo cha mtu mmoja ni pigo kwa taifa. Kauli hii inaonyesha kwamba chama hakikujaribu kupunguza uzito wa tukio hilo wala kuonyesha kwamba kilikuwa hakioni maumivu yaliyowapata wananchi.
Katika mazingira ya kisiasa, mara nyingi vyama au viongozi wanapokabiliwa na taarifa zenye uzito kama huo hujaribu kwanza kupinga takwimu au kuhoji uhalali wa taarifa husika. Kwa upande wa Migiro, alieleza kuwa CCM haikuwa na sababu ya kupinga takwimu hizo kwa kuwa zilikuwa zimekusanywa kutoka katika vyanzo rasmi ikiwemo hospitali, Msajili wa Vizazi na Vifo pamoja na taasisi nyingine zilizohusika katika uchunguzi huo.
Kauli hiyo pia ilikwenda sambamba na msimamo wake wa kupongeza kuundwa kwa tume ya uchunguzi pamoja na kazi iliyofanywa na wajumbe wake. Alieleza kuwa chama kilichukua muda kutafakari kwa kina kabla ya kutoa msimamo wake rasmi kutokana na uzito wa tukio lenyewe. Hii inaonyesha kwamba kwa mtazamo wa CCM, suala hilo halikuchukuliwa kama jambo la kawaida bali kama tukio kubwa lililohitaji umakini wa hali ya juu.
Katika sehemu nyingine ya mahojiano hayo, Migiro alisisitiza umuhimu wa maridhiano. Hii ni hoja ambayo imekuwa sehemu ya mwelekeo wa kisiasa wa Tanzania katika miaka ya hivi karibuni chini ya Rais Samia Suluhu Hassan. Kwa mujibu wa Migiro, maridhiano si tukio la siku moja bali ni mchakato endelevu unaolenga kuimarisha mshikamano wa taifa na kuhakikisha tofauti za kisiasa hazigeuki kuwa chanzo cha migawanyiko ya kudumu katika jamii.
Alijibu pia madai ambayo yamekuwa yakitolewa mara kwa mara na baadhi ya wadau wa siasa kwamba vyombo vya dola vinafanya kazi kwa maslahi ya CCM. Katika majibu yake, alisisitiza kuwa taasisi hizo ni za taifa na zinawahudumia Watanzania wote bila kujali itikadi zao za kisiasa. Wapo watakaokubaliana na maelezo hayo na wapo watakaopinga, lakini kilicho muhimu ni kwamba alitoa majibu ya moja kwa moja kuhusu suala hilo badala ya kulikwepa.
Kinachopaswa kueleweka ni kwamba katika siasa za ushindani, hasa pale ambapo suala linagusa hisia za wananchi, ni vigumu kupata kauli ambayo itakubalika kwa kila mtu. Kuna wakati hata hoja yenye maelezo ya kina na ushahidi wa kutosha inaweza kukataliwa kwa sababu ya tofauti za kimtazamo au kimisimamo ya kisiasa. Huu ni uhalisia wa siasa duniani kote. Vyama vinavyowania madaraka hupambana si tu kwa sera, bali pia kwa namna ya kutafsiri matukio na kuwashawishi wananchi waamini tafsiri zao.
Ndiyo maana baada ya mahojiano hayo kulijitokeza mjadala mkubwa. Wapo walioona Migiro alijibu kwa uwazi na kwa kuzingatia nafasi yake kama Katibu Mkuu wa CCM, huku wengine wakiona bado kulikuwa na maswali ambayo hayakupata majibu ya kuridhisha. Hata hivyo, jambo moja ambalo haliwezi kupingwa ni kwamba alitoa hoja zake kwa uwazi na akaeleza kwa nini CCM ilichukua misimamo mbalimbali baada ya matukio ya Oktoba 29.
Katika mfumo wa kidemokrasia, nguvu ya mjadala haipaswi kupimwa kwa ukubwa wa mashambulizi dhidi ya mtoa hoja, bali kwa ubora wa hoja zinazotolewa kujibu hoja zake. Ndiyo maana mahojiano ya Migiro yanapaswa kutazamwa kama sehemu ya mjadala mpana wa kitaifa unaohitaji hoja, ushahidi na uchambuzi wa kina badala ya jazba au mashambulizi binafsi. Mwishowe, wananchi ndiyo wanaobaki kuwa waamuzi wa mwisho wa hoja zinazowasilishwa na pande mbalimbali za kisiasa.
Maoni na ushauri- 0627869841/ 0713410676
