Na Jeremia Mwakyoma & Jeremiah Mbwambo- BMH

DODOMA – MEI 29, 2026

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) Prof. Abel Makubi amesema kuwa tofauti na ilivyozoeleka miaka mingine kumbukumbu ya kifo cha Hayati Rais Benjamin Mkapa inafanyika kwa mikutano na makongamano, mwaka huu BMH imeshirikiana na Mkapa Foundation kupeleka huduma za Afya za kibingwa bobezi kwa wananchi wa Masasi Mtwara.“BMH imebeba jina la Hayati Rais Benjamin Mkapa kutokana na mchango wake alioutoa enzi za uhai wake akiwa kama mtumishi wa Serikali na badae kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hasa mchango wake ktk sekta ya Afya, hivyo katika kumbukumbu hii ya miaka 6 bado tunaendelea kumkumbuka Mhe Mkapa na sisi BMH kwa kushirikiana na Mkapa Foundation tunawapelekea Wanamasasi Mtwara alipozaliwa Hayati Benjamin Mkapa, huduma za kibobezi za matibabu kuanzia Juni moja hadi tano (Juni 1 – 5, 2026)” alisisitiza Prof. Makubi

Aliongeza kuwa, katika kambi hiyo ya matibabu BMH itapeleka Madaktari Bingwa wabobezi wa magonjwa ya Presha na Moyo, Saratani, magonjwa ya watoto, upasuaji, kisukari na magonjwa mengine yasiyo ya kuambukiza ikiwemo figo, sikoseli na huduma za upandikizaji uloto.

Katika kuongeza ufanisi kwenye kambi hiyo ya madaktari Bingwa, Prof. Makubi amesema BMH itapeleka magari maalumu ya teknolojia za kisasa yenye vyumba vya upasuaji na vifaa mbalimbali vya matibabu, huduma ya kisasa ambayo kwa mara ya kwanza hapa nchini ilizinduliwa BMH mwaka 2025 kwa ushirikiano na shirika la SOTAC la nchini Uholanzi.

“Tunamshukuru Rais Dkt. Samia.Suluhu Hassan kwa Diplomasia nzuri aliyoiweka na Mataifa, BMH na SOTAC ya Uholanzi tumeshirikiana, tuna magari haya yanayoweza kwenda hadi vijijini kufuata Wananchi kuwapa huduma, tayari magari haya tumekwenda kutoa huduma nchini Burundi, Mkoani Singida, Zanzibar na maeneo mengine na huduma zitatolewa bure” aliongezea Prof. Makubi.Nae Mkurugenzi wa Uendeshaji wa shirika la SOTAC la Uholanzi Bw. Robert Roel Van Den Bos amesema kuwa wanamashirikiano mazuri na BMH, magari waliyonayo yametengenezwa katika namna inayowawezesha kufika katika eneo lolote hapa nchini na nje ya nchi kama walivyokwenda kutoa matibabu ya ubingwa bobezi nchini Burundi na sasa wanatazamia kwenda Masasi Mtwara na pia mipango ya kwenda nchini Malawi.