Serikali imewasilisha Bungeni Taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya nchini kwa mwaka 2025, ikiwa ni utekelezaji wa Kifungu cha 66 cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya mwaka 2015 kinachoitaka Serikali kuwasilisha taarifa hiyo kila mwaka mbele ya Bunge.
Akiwasilisha taarifa hiyo, Serikali imesema lengo la taarifa hiyo ni kuonesha uwajibikaji kwa wananchi kupitia Bunge pamoja na kutoa tathmini ya utekelezaji wa mikakati ya kudhibiti dawa za kulevya nchini kwa mwaka husika.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa mwaka 2025 bangi iliendelea kuwa dawa ya kulevya iliyokamatwa kwa kiwango kikubwa zaidi ambapo tani 1,017.26 zilikamatwa nchini. Hata hivyo, kiwango hicho kimepungua kwa asilimia 55.97 ikilinganishwa na mwaka 2024 kutokana na uteketezaji wa mashamba makubwa ya bangi uliofanyika mwaka 2024 pamoja na kuimarika kwa udhibiti na utoaji wa elimu kwa jamii kuhusu madhara ya kilimo hicho.
Aidha, Serikali ilikamata tani 26.36 za mirungi, kiwango kilichoongezeka kwa asilimia 42.88 ikilinganishwa na mwaka 2024, hali iliyoelezwa kuwa ni matokeo ya kuimarika kwa operesheni za ufuatiliaji na udhibiti katika maeneo ya mipaka na njia zinazotumika kusafirisha dawa hizo.
Kwa upande wa dawa za kulevya za viwandani, Serikali ilifanikiwa kukamata kilogramu 907.18 za methamphetamine, kilogramu 672.23 za heroin, kilogramu 4.89 za cocaine, gramu 178 za MDMA pamoja na gramu 7.82 za MDA.
Katika hatua nyingine, Serikali imeeleza kuwa kwa mara ya kwanza mwaka 2025 ilikamata tani 29.52 za aina mpya ya dawa za kulevya aina ya Kratom inayotokana na mmea uitwao Mitrogyna speciosa. Dawa hiyo iliingizwa nchini ikiwa imeelezwa kuwa ni mbolea, lakini uchunguzi uliofanywa ulibaini kuwa ilikuwa ni dawa za kulevya.
Serikali imeeleza kuwa mafanikio hayo yametokana na kazi kubwa inayofanywa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama katika kudhibiti mitandao na njia za usafirishaji wa dawa hizo kupitia nchi kavu, anga na majini.
Aidha, Serikali iliendelea kuimarisha ukaguzi katika vituo vya forodha, vyombo vya usafiri, kampuni za usafirishaji wa vifurushi pamoja na kampuni zinazojihusisha na biashara ya kemikali bashirifu na dawa tiba zenye asili ya kulevya kwa lengo la kudhibiti uchepushwaji wa kemikali hizo.
Kupitia ukaguzi huo, jumla ya tani 31.76 na lita 183.500 za kemikali bashirifu pamoja na kilogramu 2.36 na mililita 160 za dawa tiba zenye asili ya kulevya zilikamatwa.
Kwa upande wa mashauri ya dawa za kulevya, mwaka 2025 jumla ya mashauri 1,124 yalifunguliwa katika Mahakama mbalimbali nchini. Sambamba na mashauri yaliyokuwa yakiendelea, jumla ya mashauri 1,373 yalitolewa hukumu ambapo Jamhuri ilishinda mashauri 1,058.
Kadhalika, mali zenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 3.3 zilizohusishwa na makosa ya dawa za kulevya zilitaifishwa.
Sambamba na hatua za udhibiti, Serikali iliendelea kutoa huduma za tiba na utengamao kwa watu wenye uraibu wa dawa za kulevya ambapo mwaka 2025 jumla ya watu 85,425 walipata huduma hizo kupitia vitengo vya afya ya akili katika hospitali za rufaa za mikoa na kanda, kliniki za MAT pamoja na nyumba za upataji nafuu nchini.
Serikali pia iliendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu madhara ya dawa za kulevya kupitia kampeni mbalimbali za uelimishaji katika jamii, taasisi za elimu na vyombo vya habari kwa lengo la kujenga uelewa na uwezo wa kujilinda dhidi ya matumizi na biashara ya dawa hizo.
Katika taarifa hiyo, Serikali imeeleza kuwa mafanikio yaliyopatikana katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya yametokana na dhamira thabiti na uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, , ambaye ameendelea kuwekeza nguvu kubwa katika mapambano hayo.
Serikali pia imepongeza Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, vyombo vya ulinzi na usalama, wataalamu wa afya, wadau mbalimbali pamoja na wananchi kwa ushirikiano wao uliochangia mafanikio hayo.
Aidha, wananchi wamehimizwa kuendelea kutoa taarifa kwa vyombo husika pale wanapobaini viashiria vya biashara au matumizi ya dawa za kulevya ili kuendelea kuifanya Tanzania kuwa salama dhidi ya matumizi na biashara ya dawa hizo.

