KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Asha-Rose Migiro amesema chama hicho kilichukua muda kutafakari kwa kina matukio yaliyotokea Oktoba 29 mwaka jana kabla ya kutoa msimamo wake rasmi kuhusu ripoti ya tume ya uchunguzi iliyoongozwa na Jaji Chande.
Migiro alisema uamuzi huo ulitokana na uzito wa tukio hilo ambalo halijawahi kushuhudiwa kwa kiwango hicho katika historia ya Tanzania, hivyo chama kiliona umuhimu wa kupitia kwa makini taarifa na mapendekezo yaliyotolewa na tume hiyo.
Akizungumza katika kipindi cha Kasri la Kikeke, alisema CCM iliipokea ripoti hiyo kwa umakini mkubwa kwa kuwa ilikuwa sehemu muhimu ya kutafuta ukweli wa yaliyotokea pamoja na kuweka msingi wa kuhakikisha matukio kama hayo hayajirudii tena nchini.
Alisema chama hicho kinaendelea kuamini kuwa maridhiano ni msingi muhimu wa kudumisha umoja, amani na mshikamano wa Taifa huku kikisisitiza kuwa juhudi za kuimarisha maridhiano zinapaswa kuwa endelevu.
“CCM itaendelea kushiriki kikamilifu katika juhudi za kuimarisha maridhiano kwa lengo la kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa nchi yenye amani, mshikamano na ustawi kwa wananchi wake wote,” alisema Migiro.
Aidha, alipongeza kuundwa kwa tume ya uchunguzi pamoja na kazi iliyofanywa na wajumbe wake kwa weledi mkubwa huku akiwashukuru wananchi waliojitokeza kutoa ushahidi na maoni yao yaliyosaidia kukamilika kwa uchunguzi huo.
Alisema ushiriki wa wananchi umeonesha uzalendo na imani waliyonayo katika kutafuta suluhisho la kudumu kwa mustakabali wa taifa.
Kuhusu vifo vilivyotajwa katika ripoti hiyo, Migiro alisema CCM imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya zaidi ya watu 500 kupoteza maisha na kusisitiza kuwa hata kifo cha mtu mmoja ni pigo kubwa kwa taifa.
Alieleza kuwa chama hakina sababu ya kupinga takwimu zilizotolewa na tume kwa kuwa zimetokana na taarifa kutoka hospitali, Msajili wa Vizazi na Vifo pamoja na vyanzo vingine rasmi.
Akizungumzia vyombo vya ulinzi na usalama, Migiro alisema taasisi hizo zilifanya kazi kubwa kuhakikisha nchi inaendelea kuwa salama wakati wa matukio hayo licha ya changamoto zilizojitokeza.
Alisema jukumu lao la msingi ni kulinda usalama wa raia na mali zao pamoja na kuhakikisha taifa linaendelea kuwa na utulivu wakati wote.
“Pamoja na dosari zilizoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wa majukumu yao, bado kazi kubwa iliyofanywa na vyombo vya dola ilisaidia kuzuia madhara makubwa zaidi ambayo yangeweza kulitikisa taifa,” alisema.
Migiro pia alikanusha madai kuwa vyombo vya dola vinafanya kazi kwa maslahi ya kisiasa ya CCM akisisitiza kuwa taasisi hizo ni za taifa na zinawahudumia Watanzania wote bila kujali itikadi zao za kisiasa.
Aliongeza kuwa kipindi chote cha kampeni za uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka jana kulikuwa na hali ya utulivu na vyama vyote vilifanya shughuli zao kwa amani kufuatia wito wa Rais na Mwenyekiti wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan wa kufanya siasa za kistaarabu.
