Na Silivia Amandius 

Bukoba.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kagera imewaomba madiwani kushiriki katika mpango wa “TAKUKURU Rafiki” unaolenga kuzuia rushwa kwa njia ya mazungumzo, ushirikiano na utatuzi wa kero kabla hazijawa kubwa katika miradi ya maendeleo.

Akizungumza katika semina iliyowakutanisha madiwani, watendaji na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kagera, Leonard Swai, alisema mpango huo unalenga kufuatilia changamoto za miradi mapema na kuondoa mianya ya rushwa kabla ya miradi kufikia hatua za mwisho. Amesema mara nyingi malalamiko hutolewa kuchelewa jambo linalosababisha hasara na migogoro isiyo ya lazima.

Swai amesema viongozi wanapaswa kushirikiana kwa karibu ili kuzuia wananchi kupitia kero zisizo na majibu na kusisitiza kuwa si lazima kila jambo lifikishwe mahakamani ikiwa linaweza kutatuliwa kwa njia ya maelewano na ushauri. Aidha aliwataka madiwani na watendaji kusimamia vizuri ukusanyaji wa mapato ya ndani na kuacha tabia ya ubadhirifu wa fedha za halmashauri.

Kwa upande wao baadhi ya madiwani walieleza kuwa semina hiyo imewaongezea uelewa kuhusu mapambano dhidi ya rushwa na umuhimu wa kushirikishwa kikamilifu katika usimamizi wa miradi ya maendeleo ili waweze kubaini changamoto na vitendo vya rushwa mapema na kusaidia miradi kukamilika kwa wakati.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Fatina Hussein Laay, alisema mpango wa TAKUKURU Rafiki ni muhimu kwa kuwa unasaidia kufanya uchambuzi wa changamoto na kuamua zipi zinahitaji hatua za kisheria na zipi zinaweza kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo. Ameishukuru TAKUKURU kwa kutoa mafunzo hayo kwa madiwani ambao ni wasimamizi wakuu wa maendeleo katika kata zao.