Mkurugenzi wa Kampuni ya HAIPPA akizungumza kwenye uzinduzi wa jukwaa la TanzaniaTuwekeze

Na Hellen Mtereko,Mwanza

Jukwaa la Tanzania Tuwekeze lililoandaliwa na Kampuni ya Umma ya Kitanzania (HAIPPA PLC) limezinduliwa rasmi mkoani Mwanza.

Jukwaa hilo lenye kauli mbiu isemayo “Dira mpya – Fursa mpya; Jifunze,onyesha,uza,wekeza limezinduliwa leo Alhamis Mei 28, 2025

Tanzania tuwekeze ni jukwaa la elimu ya uwekezaji linalolenga kuwafikia watanzania milioni 20 na kuwapa elimu ya fursa za uwekezaji zinazowawezesha kuyafikia malengo ya Dira 2050 sambamba na kusaidia kukuza biashara kuwa makampuni makubwa ya Tanzania.

Akizungumza katika uzinduzi huo Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya HAIPPA, Boniface Ndengo amesema jukwaa hilo linaundwa kuwaleta pamoja wadau mbalimbali ili kuunganisha nguvu kuchochea kasi ya uwekezaji na ukuzaji biashara Tanzania.

Amesema utekelezaji wa shughuli za jukwaa hilo unatarajiwa kuzaa matokeo chanya ikiwemo kuwa na umma ulioelimishwa vema kuhusu dhana ya uwekezaji na fursa za uwekezaji zilizopo Tanzania.

Pia kuwa na umma unaoshiriki vema kwenye shughuli za uwekezaji,kuzaliwa kwa makampuni makubwa kwenye sekta mbalimbali za kiuchumi ambayo yatakuwa soko mahususi kwa wazalishaji,wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo.

“Kuunganisha nguvu za wadau ili kushirikiana kuchochea ubunifu,biashara na uwekezaji,kuzalisha fursa mpya za ajira zinazotokana na kuchochea ubunifu,biashara na uwekezaji”, Amesema Ndengo

Aidha, amesema jukwaa hilo linatarajiwa kufungua fursa maalum kwa washiriki ambao ni pamoja na vijana,wabunifu,wajasiriamali,makampuni na taasisi wadau ikiwa ni pamoja na kujifunza fursa mpaya za uwekezaji.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chemba ya biashara,Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) Mkoa wa Mwanza, Gabriel Kenene amesema HAIPPA itasaidia kuchochea kwa kiasi kikubwa uboreshaji wa maonesho ya wafanyabiashara mkoani humo.

Naye Nyihita Nyihita ambaye ni mbunifu wa kiwanda cha kusindika mafuta ya alizeti kutoka Mkoa wa Mara, amesema alianzisha kiwanda kwajili ya kupeleka fursa kwa wananchi wa maeneo hayo ili waweze kupata msukumo wa kulima zao hilo ambalo limekuwa na tija kubwa katika kukuza uchumi wa vijana wa vijijini.

Akizindua Jukwaa hilo Meneja wa Kanda ya ziwa kutoka Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), Phina Jerome amesema Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara kwakuhakikisha kunaupatikanaji wa huduma za uwekezaji kwa urahisi zaidi ikiwemo utoaji wa vivutio mbalimbali vya kiuwekezaji.

Amesema anaimani kupitia jukwaa hilo wataendelea kuona ongezeko la miradi ya uwekezaji kutoka kwa vijana,wanawake na wajasiriamali.