Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Bungeni Dodoma

Wizara ya  Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,   imeomba kuidhinishiwa jumla ya Shilingi bilioni 210.2 kwa ajili ya kutekeleza vipaumbele mbalimbali vya sekta ya ardhi katika mwaka wa fedha 2026/2027.Dkt.Akwilapo Amebainisha kuwa fedha hizo zitaelekezwa katika matumizi ya kawaida pamoja na utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayolenga kuimarisha huduma za ardhi, upangaji miji, upimaji wa viwanja pamoja na utatuzi wa migogoro ya ardhi nchini.

Dkt. Akwilapo ameyasema hayo leo Mei 28, 2026 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.Amesema kuwa kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 100.2 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida huku Shilingi bilioni 110 zikielekezwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya sekta hiyo muhimu kwa ustawi wa wananchi na ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Aidha, ameongeza kuwa fedha za maendeleo zinajumuisha Shilingi bilioni 44.1 za ndani pamoja na Shilingi bilioni 65.9 kutoka vyanzo vya nje kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya ardhi nchini.

Pia amebainisha kuwa Wizara itaendelea kuweka nguvu katika upimaji wa viwanja, usimamizi wa mipaka ya vijiji, kuimarisha mifumo ya kidijitali ya e-Ardhi pamoja na kuongeza kasi ya upangaji wa matumizi bora ya ardhi.