Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Bungeni Dodoma

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo amesema kuwa Serikali imeanza kutekeleza Programu Maalum ya Uendelezaji Upya wa Maeneo Chakavu katika miji mbalimbali nchini.

Amebainisha kuwa programu hiyo inalenga kuboresha makazi ya wananchi, kuongeza thamani ya miji pamoja na kuvutia wawekezaji katika maeneo ya mijini.Dkt. Akwilapo ameyasema hayo leo Mei 28, 2026 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Amesema kuwa jumla ya maeneo 111 yenye ukubwa wa hekta 24,309.3 yameainishwa katika halmashauri 35 zilizopo kwenye mikoa 25 nchini.

Aidha, ameongeza kuwa Serikali imeanza utekelezaji wa mradi wa mfano katika eneo la Makangira-Msasani wilayani Kinondoni kwa kushirikisha wananchi wa eneo hilo.Pia amebainisha kuwa Serikali itaendelea kupanga na kupima maeneo hayo sambamba na kutafuta wawekezaji wenye uwezo wa kuendeleza maeneo hayo kwa viwango vya kisasa.