Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Bungeni Dodoma
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Deogratius Akwilapo amesema kuwa Wizara imepanga kuhakiki, kuhuisha na kupima mipaka ya vijiji 226 katika mwaka wa fedha 2026/2027.
Amebainisha kuwa zoezi hilo linalenga kuimarisha usimamizi wa mipaka ya kiutawala pamoja na kupunguza migogoro ya ardhi vijijini.
Dkt. Akwilapo ameyasema hayo leo Mei 28, 2026 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Amesema kuwa hadi Mei 15, 2026 jumla ya vijiji 189 vilikuwa vimepimwa huku vijiji 54 vikihakikiwa na kuhuishwa mipaka yake.
Aidha, ameongeza kuwa jumla ya vijiji 11,996 kati ya vijiji 12,333 vilivyopo nchini tayari vimepimwa hatua inayosaidia kuongeza utambuzi wa mipaka halali.
Pia amebainisha kuwa Serikali za Vijiji zinapaswa kuheshimu haki za wananchi katika matumizi ya ardhi ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima.
