Na Mwandishi wetu, Mirerani
TAASISI ya Ahsante Foundation Tanzania imechinja ng’ombe 723, mbuzi na kondoo 2,500 na kutoa sadaka kwa watoto yatima, wajane, wahitaji na taasisi za serikali na binafsi, katika kusheherekea sikukuu ya Eid Al-Adha mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara.
Meneja mipango wa taarifa ya Ahsante Foundation Tanzania, Omary Gyunda amesema lengo ni kuhakikisha jamii yenye mahitaji inanufaika na sadaka ya sikukuu hiyo ya Idd.
Gyunda amesema taarifa ya Ahsante Foundation Tanzania wamechinja ng’ombe 723, mbuzi na kondoo 2,500 kwa ajili ya jamii kushiriki sherehe hiyo bila ubaguzi wa madhehebu katika mji mdogo na maeneo ya jirani.
Amesema sadaka hiyo ya nyama ya kuchinja imetolewa kwa watoto yatima, wajane, wahitaji mbalimbali na taasisi za serikali na binafsi za mji mdogo wa Mirerani na majirani zao.
“Tumetoa sadaka hiyo ya kuchinja kwa wahitaji hao na taasisi mbalimbali ikiwemo shule za msingi, sekondari, polisi, uhamiaji, zimamoto na mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani,” amesema Gyunda.
Ameeleza kwamba shughuli ya kuchinja wanyama na kugawa kwa wahitaji imekuwa endelea kwani imefanyika kwa zaidi ya muda wa miaka minne katika mji mdogo wa Mirerani na majirani wa eneo hilo.
Amesema taasisi hiyo inajihusisha na kusaidiana jamii katika matukio mbalimbali ikiwemo kuwapatia futari waumini wanapofunga katika ibada.
“Pia tumekuwa tukisaidia kuchimba visima katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kuondoa changamoto ya ukosefu wa maji,” amesema Gyunda.