Na Mwandishi Wetu, Pwani

WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umesema maboresho ya miundombinu yanayotekelezwa kupitia Mradi wa Kujenga Ustahimilivu wa Bioanuwai ya Misitu dhidi ya Athari za Mabadiliko ya Tabianchi katika Misitu ya Asilia ya Hifadhi Tanzania (BUREFOBI-NFR), yamechochea ukuaji wa utalii ikolojia katika Hifadhi ya Msitu wa Asili wa Pugu Kazimzumbwi, mkoani Pwani.

Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali kufikia lengo la kuongeza idadi ya watalii hadi milioni nane ifikapo mwaka 2030 kupitia uboreshaji wa vivutio na huduma za utalii nchini.

Akizungumza wakati wa ziara ya Mshauri wa Kanda wa Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Onesimus Muhwezi, Mratibu wa Mradi wa BUREFOBI-NFR ambaye pia ni Mhifadhi Mkuu wa TFS, Someni Mteleka, alisema uwekezaji huo umeongeza mvuto wa hifadhi hiyo kwa watalii wa ndani na nje ya nchi.

Alisema kupitia ufadhili wa pamoja wa Mfuko wa Mazingira Duniani (GEF) na UNDP, TFS imetekeleza miradi mbalimbali ya kuboresha miundombinu ya utalii katika hifadhi hiyo, ikiwemo ujenzi wa barabara ya kilomita 12 katika eneo la Kimani–Maguruwe, mabanda mawili ya kupumzikia watalii pamoja na lango la kuingilia hifadhini.

“Uboreshaji huu umeongeza upatikanaji wa huduma na kurahisisha watalii kufikia maeneo mbalimbali ya vivutio ndani ya hifadhi,” alisema Mteleka.

Alibainisha kuwa kati ya mwaka 2020 na 2025, Hifadhi ya Pugu Kazimzumbwi imerekodi ongezeko la wastani wa watalii kwa asilimia 69, hali aliyosema imechangiwa na uwekezaji katika miundombinu ya utalii ikolojia na ushirikiano kati ya Serikali na washirika wa maendeleo.

Kwa upande wake, Muhwezi aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa kupitia ufadhili wa washirika wa kimataifa, akisema miradi hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika uhifadhi wa mifumo ya ikolojia, kukuza uchumi wa jamii zinazozunguka hifadhi pamoja na kuongeza mapato yatokanayo na utalii.

Hifadhi ya Msitu wa Asili wa Pugu Kazimzumbwi ni miongoni mwa hifadhi tisa zinazotekelezwa mradi wa BUREFOBI-NFR, unaolenga kuimarisha ustahimilivu wa bioanuwai ya misitu dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi nchini.