Na. Dennis Gondwe, DODOMA

WANANCHI wa Wilaya ya Dodoma wameombwa kuonesha umoja na mshikamano wao kwa kujitokeza kwa wingi kuupokea na kuukimbiza Mwenge wa Uhuru utakapowasili na kutembelea miradi ya maendeleo inayolenga kuboresha maisha yao.

Kauli hiyo ilitolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Vincent Odero alipokuwa akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu maandalizi ya mapokezi ya Mwenge wa Uhuru Mwaka 2026 katika Wilaya ya Dodoma.

Alisema kuwa Mwenge wa Uhuru ni chombo cha umoja na mshikamano ambao umekuwa ukitafsiriwa kwa vitendo wilayani Dodoma. “Wilaya ya Dodoma tumekuwa tukionesha umoja na mshikamano wa wazi linapokuja suala ya Mwenge wa Uhuru kwa miaka yote. Hili ni jambo la heshima kwetu. Nitumie nafasi hii kuwaalika na kuwaomba tena wananchi wote tarehe 1 Juni, 2026 kuupokea Mwenge wa Uhuru katika Mtaa wa Vikonje B, Kata ya Mtumba na kuukimbiza katika miradi yote ya maendeleo na kushiriki mkesha mkubwa utakaofanyika katika uwanja Shule ya Msingi Kizota” alisema Odero.

Mwenge wa Uhuru umekuwa chachu ya kuhamasisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo. “Kwa kuzingatia kaulimbiu isemayo ‘Tanzania ni yetu sote, tushikamane kwa pamoja kuleta maendeleo’ inasadifu lengo la Mwenge wa Uhuru la kuleta maendeleo kwa wananchi wa Wilaya ya Dodoma kwa kuhamasisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi. Sisi tunaamini kuwa maendeleo ni mchakato wa pande zote, hivyo, umoja wetu na mshikamano wetu ndiyo msingi wa maendeleo yetu” alisema Odero.

Akiongelea falsafa ya Mwenge wa Uhuru alisema kuwa imejengeka katika misingi ya haki, usawa, umoja na uwajibikaji. “Mwenge wa Uhuru umetoa mchango mkubwa kwa kuchochea maendeleo ya Wilaya ya Dodoma, amani, utulivu, mshikamano na umoja wa kitaifa. Kikubwa zaidi umekuwa ukihamasisha kupambana na vitendo vya rushwa, uzembe, matumizi mabaya ya rasilimali za umma” alisema Odero.

Wakati huohuo, aliwakaribisha vijana wa wilaya ya Dodoma kujitokeza kwa wingi katika kongamano la vijana. “Mwenge wa Uhuru, utatanguliwa na kongamano ya vijana litakalofanyika kwa siku mbili tarehe 29-30 Mei, 2026. Kongamano hilo ni fursa kwa vijana kujifunza mambo mbalimbali kuanzia elimu ya uraia, uzalendo, hadi fursa za kiuchumi kwa vijana” alisema Odero.

Nae mkazi wa Wilaya ya Dodoma, Mariam Omary alisema kuwa Mwenge wa Uhuru umekuwa ukihamasisha umoja na mshikamano kwa wananchi wote kwa sababu unawaunganisha na kuchochea maendeleo.

MWISHO