Na Mwandishi Wetu, Siha
Mkuu wa Wilaya ya Siha, Dkt. Christopher Timbuka, amezindua rasmi mashindano ya West Kili Forest Tour Challenge yanayotarajiwa kuvutia zaidi ya washiriki 800 kutoka ndani na nje ya nchi, huku yakilenga kutangaza utalii, kuhamasisha michezo na kuchochea ukuaji wa uchumi kwa wananchi wa Wilaya ya Siha.
Mashindano hayo yatafanyika Juni 20 hadi 21, 2026 katika ukanda wa msitu wa West Kilimanjaro na yatahusisha mbio za kilomita 5, 10 na 21, sambamba na mashindano ya baiskeli na pikipiki yatakayopita katika mandhari ya kuvutia ya msitu huo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Mei 26,2026, Dkt. Timbuka amesema tukio hilo ni fursa muhimu ya kuitangaza Siha kama kitovu cha utalii wa asili na michezo, huku likitoa nafasi kwa wananchi kunufaika kiuchumi kupitia biashara mbalimbali zitakazoambatana na mashindano hayo.
Amesema maandalizi yamekamilika kuhakikisha mashindano hayo yanafanyika kwa mafanikio makubwa na kuwa sehemu ya matukio muhimu ya utalii na michezo nchini.
Aidha, waandalizi wameeleza kuwa kabla ya siku ya mashindano kutafanyika mkesha maalumu wa burudani utakaowakutanisha washiriki, wadau na wananchi kupitia shughuli mbalimbali za kijamii, chakula, vinywaji na burudani kuelekea siku kuu ya mashindano.
Mashindano hayo yanaungwa mkono na kampuni za Mati Super Brands Ltd, Bonite Bottlers Ltd, Notice Kilimanjaro, CYCA Tanzania na Solo Adventures ambazo zimeahidi kushirikiana kuhakikisha tukio hilo linafanyika kwa mafanikio makubwa na kuwa la kipekee.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Siha, Dkt. Godwin Molel, amesema ataendelea kuhamasisha wananchi, wadau na marafiki zake kushiriki katika mashindano hayo ili kuongeza chachu ya utalii na uchumi katika eneo hilo.
Amesema atashirikiana na kampuni ya Zara Tours pamoja na taasisi za TATO na TLTO kuwakaribisha mawakala na makampuni ya utalii kutembelea eneo hilo na kujionea fursa mbalimbali za utalii zilizopo ndani ya hifadhi.
Kwa mujibu wa Mhifadhi Mkuu wa Pori la Akiba West Kilimanjaro, Robert Faida, West Kili Forest Tour Challenge si mashindano ya michezo pekee, bali ni jukwaa muhimu la kutangaza vivutio vya utalii vya West Kilimanjaro na kuhamasisha uhifadhi wa mazingira kupitia michezo na utalii endelevu.

