Na Mwandishi Wetu – Msumbiji
SERIKALI imesema inaendelea kujipanga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha utafiti katika kukabiliana na majanga katika ukanda wa Kusini mwa Afrika (SADC) na Afrika Mashariki, hatua itakayosaidia kuimarisha mifumo ya tahadhari na uokoaji.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Dkt. Jim Yonazi, wakati wa ziara ya kubadilishana uzoefu kati ya Tanzania na Msumbiji kuhusu hatua za mapema kabla ya majanga.
Ziara hiyo ya siku tano inayofanyika jijini Maputo nchini Msumbiji kuanzia Mei 25 hadi 29, 2026, inalenga kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu matumizi ya teknolojia za kisasa, tafiti na mifumo ya utoaji wa taarifa za tahadhari mapema ili kupunguza athari za majanga.
Akizungumza katika mkutano huo, Dkt. Yonazi alisema Tanzania imeendelea kujenga uwezo wake katika kukabiliana na majanga kupitia uwekezaji katika tafiti na matumizi ya teknolojia za kisasa ikiwemo mifumo ya kidijitali na akili bandia (AI), hali inayoifanya nchi kuwa kivutio kwa mataifa mengine kujifunza.
Alisema Serikali imeweka mkazo katika kuimarisha mifumo ya kisayansi na TEHAMA ili kuhakikisha taarifa za mapema zinapatikana kwa wakati na kusaidia kuchukua hatua stahiki kabla ya majanga kutokea.
“Tumekaa na kujadili namna ya kuendeleza ushirikiano kati ya nchi yetu na Msumbiji. Dhamira yetu ni kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha utafiti na kukabiliana na majanga katika ukanda wa SADC na Afrika Mashariki,” alisema.
Aliongeza kuwa tayari hatua mbalimbali zimeanza kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kuimarisha mifumo ya kitaifa ya kukabiliana na majanga ikiwemo kutumia teknolojia za kisasa.
Aidha, ameeleza kuwa kumekuwepo na mpango maalum wa ushirikiano na Taasisi za elimu ya Juu na Taasisi za Utafiti zilizopo nchini katika kufanya tafiti na kujenga mifumo itakayowezesha kujenga uwezo wa nchi ya Tanzania kukabiliana na Maafa.
Dkt. Yonazi alisisitiza kuwa Tanzania ina nia ya kuvutia nchi nyingine za Afrika Mashariki na SADC kuja kujifunza na kushirikiana katika masuala ya tafiti, teknolojia na mbinu za kisasa za kukabiliana na majanga.
Alibainisha kuwa mkakati huo ni sehemu ya jitihada za Serikali kuhakikisha inalinda maisha ya wananchi, mali zao pamoja na kuendelea kuhifadhi na kusambaza maarifa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Katika mkutano huo, ajenda kuu ilikuwa ni kuweka mikakati ya kuchukua tahadhari mapema dhidi ya majanga badala ya kusubiri yatokee ndipo hatua zichukuliwe, hatua ambayo imeelezwa kuwa ni msingi muhimu wa sera ya Serikali katika usimamizi wa maafa.

