*Ni sehemu ya jitihada za kuwaongezea uwezo wa ulinzi wa miundombinu

Viongozi waandamizi wa Jeshi la Polisi nchini wamefanya ziara ya kutembelea miundombinu mbalimbali ya gesi asilia inayosimamiwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuwaongezea uwezo kuhusu usimamizi na ulinzi wa miundombinu ya kimkakati ya taifa.

Ziara hiyo imehusisha viongozi mbalimbali wa Jeshi la Polisi wakiwemo Makamanda wa Wilaya (OCDs) pamoja na makamanda kutoka mikoa yote yenye miundombinu ya gesi asilia nchini.

Viongozi hao wametembelea miundombinu ya kupokelea gesi asilia katika eneo la Kinyerezi jijini Dar es Salaam, ambapo wamepata maelezo kuhusu shughuli zinazotekelezwa katika eneo hilo pamoja na umuhimu wa miundombinu hiyo katika kuhakikisha upatikanaji wa nishati nchini.

Aidha, wametembelea Kituo Mama cha Kujaza Gesi Asilia kwenye Magari (CNG Mother Station) kinachomilikiwa na TPDC kilichopo eneo la Mawasiliano jijini Dar es Salaam, ambapo wamejionea namna teknolojia ya matumizi ya gesi asilia kwenye magari inavyotekelezwa pamoja na mchango wake katika matumizi ya nishati safi, salama na yenye gharama nafuu.

Ziara hiyo inaendelea kwa kutembelea miundombinu mingine muhimu ikiwemo bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, Kiwanda cha Kuchakata Gesi Asilia cha Madimba mkoani Mtwara pamoja na visima vya kuzalisha gesi asilia vilivyopo Kata ya Msimbati.