Na. Calvin Katera – Babati.
Bondia maarufu duniani toka nchini Marekani Terence “Bud” Crawford amejikuta katika bashasha kubwa ndani ya Hifadhi ya Taifa Tarangire mara baada ya kupokelewa na burudani kutoka kikundi cha watumbuizaji wa nyimbo za jamii ya kimasai leo Mei 26, 2026 mjini Babati.
Akiwasili hifadhini hapo Crawford alikutana na menejimenti ya hifadhi na kupata maelezo mafupi juu ya vivutio vinavyoipa umaarufu hifadhi hiyo kitaifa na kimataifa sambamba na matayarisho yanayofanywa kupokea wageni katika kipindi cha michuano ya mpira wa miguu barani Afrika, AFCON 2027.
Akiongoza mapokezi hayo Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Tarangire Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Tutindaga Mwakijembile alieleza kuwa ujio wa watu mashuhuri duniani katika vivutio vyetu imekuwa chachu ya kutangaza utalii kitaifa na kimataifa na hasa kipindi hiki tunachojiandaa na mashindano ya AFCON mwakani.
“Vivutio vyetu vimekuwa vikijitangaza kupitia watalii wanaotutembelea hifadhini hasa pale watu mashuhuri wanapokuja thamani yake katika mipaka ya kimataifa huongezeka zaidi na ukizingatia msimu huu tunaanda mashindano makubwa barani Afrika” alisema Kamishna Tutindaga.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Habari kutoka Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Pauline Mkama alieleza kuwa ujio wa Crawford hautoishia ndani ya Hifadhi ya Taifa Tarangire pekee, badala yake utavuka mipaka na kufika Serengeti mahala ambako atapata taswira mpya ya utalii na uhifadhi.
Terence Crawford anasifika kwa rekodi yake ya kushinda mechi za masumbwi 42 bila kupoteza hata mchezo mmoja, huku michezo 31 akipata ushindi wa mapema (knockouts -KO). Ziara inatazamiwa kuwaalika wapiganaji wengine toka nje ya mipaka ya Tanzania kuja kufanya mapumziko, kupata burudani, na kujinoa ndani ya maeneo ya asili yanayoshahabiana na michezo yao.

