BENKI ya CRDB imeonyesha nia ya kufadhili kituo cha michezo na malezi ya vijana cha Fountain Gate Academy kilichopo Dodoma kwa vifaa mbalimbali zikiwemo jezi za wachezaji kwa muhula ujao wa masomo.
Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela ametoa kauli hiyo baada ya kutembelea Shule za Fountain Gate kampasi ya Dodoma kwa lengo la kuangalia maendeleo ya uwekezaji wa shule hizo ikiwemo academy ya kutambua vipaji, kufundisha na kuwalea vijana kisoka.
Pia Nsekela amewataka vijana wanaolelewa katika kituo cha Fountain Gate Academy kuwa na nidhamu na kuonyesha tabia njema wawapo kituoni na nje ya kituo.
“Mpira ni elimu na kwa bahati nzuri mna walimu ningekuwa naishi Dodoma ningehamia hapa kwa sababu mimi ni mchezaji mzuri sana, nilikuwa miongoni mwa wachezaji wakubwa sana mkoani Kagera enzi hizo” Alisema Nsekela.
“Sisi kama CRDB tunashukuru sana kwa kuwa wateja wetu wazuri na tutaendelea kushirikiana pale inapobidi ili kuendelea kujenga umoja na utamaduni kutangaza mashirika yetu mawili ya Fountain Gate na CRDB”. Aliongeza Nsekela
Ziara hiyo imekuja baada ya mwaliko kutoka kwa Mkurugenzi wa Fountain Gate Academy Japhet Makau kumuomba kutembelea kampasi hiyo ya Dodoma kuangalia uwekezaji uliofanywa na shule hizo na kutambua fursa mbalimbali kama moja ya wadau wakubwa wa maendeleo mkoa wa Dodoma na Tanzania.
Naye Mkurugenzi wa Fountain Gate Academy Japhet Makau amesema kituo chake kimelenga kuendeleza vipaji vya mpira mkoani Dodoma na Tanzania lakini wanawapa vijana fursa ya kujifunza ujasiliamali.
“Tayari vijana wetu wanaweza kutengeneza sabuni, kutengeneza batiki na tupo hatua za mwisho kukamilisha ufunguaji wa bustani kubwa ili wajifunze kilimo cha mbogamboga”. Alisema Makau
Fountain Gate Academy inakamilisha ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu hadhi ya kimataifa kwa ajili ya kuwezesha kituo cha michezo cha Fountain Gate Academy kuwa kitovu cha mafunzo kitaifa na kimataifa.