WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amewasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Maya Maya jijini Brazzaville, nchini Jamhuri ya Kongo kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa 61 wa Mwaka wa Bodi ya Magavana wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).

Dkt. Mwigulu anamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mkutano huo utakaofanyika Mei 26 hadi 27, 2026 katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Kintele jijini Brazzaville.

Akiwasili nchini humo, Dkt. Mwigulu alipokelewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kongo, Anatole Collinet Makosso.

Mkutano huo ni jukwaa muhimu la majadiliano ya kimkakati kuhusu masuala mbalimbali ya maendeleo duniani ukiwahusisha viongozi wa nchi wanachama, taasisi za kikanda na kimataifa kwa lengo la kuhamasisha upatikanaji wa rasilimali za fedha ili kuwezesha utekelezaji wa ajenda ya maendeleo ya Afrika na kuimarisha uwezo wa bara hilo kukabiliana na changamoto za kiuchumi na kifedha duniani.

Mkutano huo unatarajiwa kuwakutanisha wajumbe wapatao 3,000 wakiwemo Wakuu wa Nchi, Mawaziri wa Fedha, Magavana wa Benki Kuu za Afrika, watunga sera, wafanyabiashara, taasisi za kifedha, washirika wa maendeleo, wajasiriamali pamoja na wawekezaji.