Na.Sophia Kingimali.

Rais wa Shirikisho la vyama vya wafanyakazi nchini (TUCTA), Tumaini Nyamhokya, amewataka wanahabari nchini kujiunga na vyama vya wafanyakazi ili kujenga umoja, kulinda maslahi yao na kupigania haki zao mahali pa kazi kwani kupitia umoja huo waandishi wa habari wataweza kupata nguvu ya pamoja katika kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo ukosefu wa mikataba ya ajira na mazingira magumu ya kazi.

Akizungumza leo Mei 25 katika mafunzo yaliyoandaliwa kwa kushirikiana kati ya JOWUTA na Mfuko wa fidia kwa wafanyakazi (WCF), Nyamhokya amesema vyama vya wafanyakazi vina mchango mkubwa katika kuhakikisha wafanyakazi wanapata haki zao na kutetea maslahi yao wanapokumbwa na changamoto kazini.

Alisema waandishi wengi wa habari wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu bila mikataba rasmi ya ajira huku wengine wakilipwa kwa kutegemea idadi ya habari wanazoandika, hali ambayo inawanyima uhakika wa maisha na mafao muhimu ya kazi.

Aidha Nyamhokya amewataka wanahabari kutumia vyama vya wafanyakazi kama sehemu ya kujenga sauti ya pamoja na kushiriki kikamilifu katika shughuli za vyama hivyo ili kuimarisha nguvu ya wafanyakazi nchini. 

“Umoja ndiyo silaha muhimu ya kupambana na unyanyasaji wa kikazi pamoja na ukosefu wa haki kwa wafanyakazi”,Amesema.

Aidha, ameipongeza WCF kwa kuendelea kutoa elimu kuhusu umuhimu wa mfuko huo kwa wafanyakazi mbalimbali nchini, akieleza kuwa wafanyakazi wengi bado hawafahamu namna mfuko huo unavyoweza kuwasaidia wanapopata madhara au ajali zinazotokana na kazi zao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa JOWUTA Mussa Juma amesema ushirikiano kati ya chama hicho na TUCTA umeanza kuzaa matunda baada ya chama hicho kupokelewa rasmi ndani ya shirikisho hilo mwaka jana mjini Singida. 

Aidha Juma amesema hatua hiyo imeongeza nguvu ya chama katika kupigania maslahi ya wanahabari nchini.

Mwenyekiti huyo amesema zaidi ya asilimia 80 ya wanahabari nchini hawana mikataba rasmi ya kazi licha ya baadhi yao kuwa na elimu kubwa ya taaluma mbalimbali, hali inayowafanya kukosa haki za msingi za wafanyakazi na kutotambulika rasmi na waajiri wao.

Amesema chama hicho kinaendelea kushirikiana na Wizara ya Kazi pamoja na Kamishna wa Kazi kuhakikisha changamoto za wanahabari zinapatiwa ufumbuzi, ikiwemo suala la mikataba ya ajira na mazingira bora ya kazi.

Naye Mkuu wa kitengo cha mahusiano kwa umma Mfuko wa fidia kwa wafanyakazi(WCF) RAULA Kunenge amesema mfuko huo utaendelea kutoa elimu kwa wanahabari na wafanyakazi wengine kuhusu haki zao wanapopata ajali au madhara yanayotokana na kazi wanazozifanya.

Amesema wanahabari ni wadau muhimu katika kufikisha elimu kwa jamii, hivyo ushirikiano kati ya WCF na JOWUTA utasaidia wananchi wengi kuelewa umuhimu wa mfuko huo na huduma zinazotolewa kwa wafanyakazi nchini.

Katika mafunzo hayo, washiriki walipata elimu kuhusu haki za wafanyakazi, umuhimu wa kujiunga na vyama vya wafanyakazi pamoja na namna ya kupata huduma za fidia kupitia WCF wanapopatwa na madhara yanayotokana na kazi zao.

Nyamhokya amesisitiza kuwa mshikamano wa wafanyakazi ndio msingi wa kupata maendeleo na haki kazini, huku akiwahimiza wanahabari kuendelea kuwa sauti ya jamii kwa kuandika habari zinazogusa maslahi ya wananchi pamoja na wafanyakazi nchini.