

…………..
Na Mwandishi Wetu, Tunduru
BAADHI ya wafanyabiashara waliopanga katika vibanda vya Halmashauri ya wilaya Tunduru Mkoani Ruvuma,wameilalamikia ofisi ya biashara ya Halmashauri hiyo kuwaongezea kodi za pango holela na baadhi ya watumishi kujimilikisha vibanda vingi na kuwanyima haki wafanyabiashara.
Wamesema hayo, wakati wa kikao cha wafanyabiashara kilichoitishwa na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Seif Dauda kwa lengo la kusikiliza kero zao kilichofanyika katika ukumbi wa Sky way mjini Tunduru.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara Boniface Pawasa alisema,ofisi ya biashara inapangisha vibanda kwa watu zaidi ya wawili kwa maslahi yao binafsi hivyo kusababisha migogoro mingi na baadhi ya wananchi wanadhulumiwa fedha zao.
“Mimi yamenikuta huyu afisa biashara kwa kushirikiana na msaidizi wake Ngai wamenidhulumu fedha zangu na kunipeleka mahakamani,huyu Ngai mtu mbaya sana,naomba uongozi wa Halmashauri watu mnaowaweka ofisini wawe na elimu ya biashara badala ya kupeana vyeo kwa kujuana”alisema Pawasa.
Aziz Komba alisema,watendaji wa Halmashauri ya wilaya wamekuwa wakwakamata na kuwashitaki wafanyabiashara hao bila kutoa nafasi ya kujitetea na wengine kuchukulia bidhaa zao na kutozwa faini kubwa kuliko mitaji na vipato vyao.
Alisema, kutokana na changamoto hiyo baadhi ya wananchi wameshindwa kuendelea kufanya biashara hivyo kuwanyima haki na kuikosesha Serikali mapato.
Katibu wa chemba ya Taifa ya biashara(TNCC)wilayani Tunduru Mohamed Kiyonjo alisema,migogoro mingi inatokana na ukiukwaji wa makubaliano yanayofanyika kati yao na halmashauri hiyo.
Alisema kuna watumishi wa Halmashauri wanamiliki vibanda zaidi ya kumi na tano na kuvipangisha kwa wafanyabiashara kwa bei kubwa tofauti na bei halali ya Halmashauri.
Kiyonjo ameshauri,kuwapokonya watu wenye vibanda vingi ili wapewe wafanyabiashara wenye uhitaji kwani kuna wapangaji wamevifunga vibanda hivyo kwa muda mrefu bila kufanya shughuli yoyote.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma Seif Dauda,amewataka watumishi wa Halmashauri hiyo kufanya kazi kwa weledi na kuwa na mahusiano mazuri ili kuepusha migogoro baina yao na wafanyabiashara.
Ametoa wito kwa watendaji wa Halmashauri hiyo,kuhakikisha wanatenda haki ili kuwawezesha wafanyabiashara walipe mapato kwa wakati,hivyo kuisaidia halmashauri kuongeza mapato na kukuza uchumi wa nchi.
Alisema,Halmashauri inategemea mapato mbalimbali kutoka kwa wananchi waliojiajiri katika sekta ya biashara,hivyo ni muhimu pande zote mbili kuendelea kushirikiana na kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria,kanuni na taratibu za nchi.
“Ni lazima tutengeneze mahusiano mazuri kati ya nyinyi watoa huduma na sisi tuliyopea dhamana ya kuisimamia jamii,tusipotengeneza mahusiano mazuri naamini Tunduru itayumba kwa sababu kila mmoja atakimbilia kutengeneza jambo lake na siyo la kwetu kwa pamoja”alisema Dauda.
Alisema,wafanyabiashara ni wadau muhimu,ndiyo maana Halmashauri inawategemea sana na kama hawatokuwa kitu kimoja hawawezi kufanikiwa kuijenga Tunduru yao na kuwaomba washirikiane kuijenga wilaya yao kwa kutumia rasilimali zilizopo ili waweze kutoa huduma bora kwa jamii.
Alisema,baadhi ya watumishi wanafanya kazi kwa mazoea,visasi na utashi binafsi hivyo kuisababishia Halmashauri kukosa mapato na kwamba mtendaji atakayebainika kufanya hivyo atachukuliwa hatua za kinidamu kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa umma.
Amewataka wafanyabiashara hususani wapangaji wa vibanda vya Halmashauri kuendelea kufanya kazi zao kwa uadilifu na kuepuka makosa na migogoro hasa ya ukwepaji kodi halali za Serikali.
Akizungumzia migogoro ya vibanda na vizimba alisema,vibanda hivyo ni mali ya Halmashauri,lakini changamoto kubwa baadhi yao wamepangisha kwa watu wengine kwa fedha nyingi na kusababisha migogoro kati ya wapangaji wa kati na halmashauri.
