NA DENIS MLOWE, IRINGA 
MKOA wa Iringa unajiandaa kwa shamrashamra za maadhimisho ya 29 ya Wiki ya Maziwa nchini, yatakayofanyika kuanzia Mei 25 hadi Juni 1, 2026 katika Viwanja vya Mwembetogwa
Hafla hiyo inatarajiwa kuvuta maelfu ya wadau wa sekta ya maziwa kutoka ndani na nje ya mkoa.
Maadhimisho hayo yanaandaliwa na Bodi ya Maziwa Tanzania kwa ushirikiano na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ikiwa na lengo la kuimarisha mnyororo wa thamani wa maziwa kuanzia uzalishaji, ukusanyaji, usindikaji hadi masoko. Wafugaji, wachakataji, taasisi za fedha na wawekezaji wanatarajiwa kujitokeza kuonesha bidhaa, teknolojia mpya na fursa za kukuza sekta hiyo.
Akitoa taarifa kuhusu maandalizi, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, alisema sekta ya maziwa imeendelea kuwa nguzo muhimu ya uchumi wa wananchi hususan katika maeneo ya vijijini, ambapo maelfu ya kaya hutegemea ufugaji wa ng’ombe wa maziwa kwa kipato na lishe.
Amesisitiza kuwa Iringa imekuwa mfano wa kuigwa katika uzalishaji wa maziwa kutokana na mazingira rafiki ya ufugaji na jitihada za Serikali kuimarisha miundombinu kupitia miradi kama ule wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabianchi (C-SDTP).
Kwa mwaka huu, kaulimbiu “Rasimisha Biashara ya Maziwa, Okoa Maisha ya Walaji, Ongeza Kipato, Changia Uchumi” inalenga kuimarisha uelewa kuhusu umuhimu wa kufanya biashara ya maziwa kwa kufuata mifumo ya kisheria pamoja na kudumisha ubora wa bidhaa.
Takwimu za sasa za Bodi ya Maziwa zinaonesha kuwa Tanzania inazalisha zaidi ya lita bilioni 4 za maziwa kwa mwaka, huku matumizi kwa mtu mmoja yakiwa lita 70 kwa mwaka kiwango ambacho bado hakijafikia wastani wa kimataifa wa zaidi ya lita 200 kwa mwaka.
Kwa upande wake Afisa Masoko wa Bodi ya Maziwa Tanzania, Joseph Semu, alisema maadhimisho haya yanatoa fursa adhimu kwa wananchi kupata elimu kuhusu unywaji wa maziwa salama, ufugaji wa kisasa na uwekezaji katika sekta inayozidi kukua kwa kasi.
Katika kipindi chote cha wiki ya maziwa, kutakuwa na maonesho ya bidhaa, usajili wa wadau, mafunzo ya usindikaji na lishe, pamoja na kampeni za kuhamasisha unywaji wa maziwa mashuleni na katika vituo vya watoto wenye mahitaji maalum. Vilevile, kongamano maalum la wataalamu wa mifugo na wawekezaji litajadili mbinu za kuongeza thamani ya maziwa na kupanua masoko nchini.
Mamlaka za mkoa zimesema zinaendelea kushirikiana na Serikali Kuu na sekta binafsi katika kuimarisha miundombinu ya uzalishaji na usindikaji ili kuongeza uzalishaji wa ndani na kupunguza utegemezi wa maziwa kutoka nje.