Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imeteketeza kilogramu 504.36 za dawa za kulevya aina ya heroin katika kiwanda cha saruji cha Dangote Cement mkoani Mtwara, kufuatia amri ya Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Mtwara baada ya kukamilika kwa hatua za kisheria dhidi ya watuhumiwa waliohusika na dawa hizo.
Dawa hizo zilikamatwa ndani ya jahazi la Al Arab lililokuwa na raia saba wa Iran katika Bahari ya Hindi ndani ya eneo la kiuchumi la Tanzania. Uteketezaji huo umefanyika kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Sura ya 95 inayoruhusu vielelezo vya dawa za kulevya kuteketezwa baada ya taratibu za kisheria kukamilika au kwa idhini ya mahakama wakati shauri linaendelea.
Sambamba na hatua hiyo, DCEA imeendelea kusisitiza umuhimu wa kuimarisha huduma za tiba na utengemao kwa watu wenye uraibu wa dawa za kulevya, hususan katika ukanda wa kusini mwa Tanzania. Katika utekelezaji wa azma hiyo, mamlaka itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuwezesha upatikanaji wa huduma za MAT pamoja na kuanzishwa kwa nyumba za upataji nafuu (sober houses) kwa lengo la kusaidia waraibu kupata huduma stahiki na kurejea katika maisha yenye tija kwa jamii.
Aidha, DCEA imeeleza kuwa itaendelea kushirikiana na vyombo vya dola, wadau pamoja na wananchi katika kuzuia usafirishaji, biashara na matumizi ya dawa za kulevya nchini. Mamlaka hiyo pia imeahidi kuendelea kuimarisha utoaji wa elimu kwa umma kuhusu madhara ya dawa za kulevya na umuhimu wa ushiriki wa jamii katika mapambano dhidi ya biashara hiyo haramu.

