šAsema mradi huo utafungua fursa mpya za uchumi na kupunguza msongamano wa magari mjini Iringa
šAagiza malipo ya vibarua yafanyike kwa wakatiĀ
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika miradi ya kimkakati ya miundombinu ili kuboresha usafiri, kuongeza ufanisi wa uchukuzi na kufungua fursa mpya za maendeleo ya kiuchumi nchini.
Amesema hayo leo Jumamosi, Mei 23, 2026 wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa Barabara ya Mchepuo ya Mji wa Iringa (Iringa Municipal Bypass) yenye urefu wa kilomita 7.3 inayojengwa kwa kiwango cha lami mkoani Iringa.
āBarabara hii ni muhimu kwa uchumi wa Mkoa wa Iringa na Taifa kwa ujumla. Itasaidia kupunguza msongamano wa magari, kuongeza biashara na kuchochea ukuaji wa mji wa Iringa,ā amesema Dkt. Nchemba.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Waziri Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kutekeleza miradi mikubwa ya barabara nchini kwa lengo la kuimarisha uchumi na kurahisisha huduma za usafiri na uchukuzi.
Amesema barabara hiyo itakuwa suluhisho la kudumu la msongamano wa magari katika mji wa Iringa hususan katika eneo la mlima wa Ipogoro ambalo limekuwa likikumbwa na ajali na changamoto za usafiri kutokana na ongezeko kubwa la idadi ya watu, magari na vyombo vingine vya usafiri.
āNdugu zangu wana Iringa, Mheshimiwa Rais amejipambanua kuwa ni Rais wa matokeo. Akisema jambo analitekeleza, na ndiyo maana mnaendelea kuona miradi mikubwa ya barabara ikitekelezwa karibu kila kona ya nchi,ā amesema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka wakandarasi wanaotekeleza miradi ya Serikali kuhakikisha wanawalipa kwa wakati wakandarasi wadogo, mafundi na vibarua wanaoshiriki katika utekelezaji wa miradi hiyo.
āKadri wanavyopata fedha, wawalipe wale wanaotekeleza mradi pamoja nao. Sio vizuri mradi ukamilike wakati wengine waliotoa huduma wanadai malipo yao,ā amesema.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa Serikali wa kujenga barabara za mchepuo katika miji mikubwa ili kupunguza msongamano wa magari na kuongeza ufanisi wa usafiri wa mizigo nchini.
Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Iringa, Mhandisi Hosea Machaka amesema utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 38.5 huku kazi mbalimbali zikiendelea ikiwemo ulipuaji wa miamba, ujazaji wa kifusi, ujenzi wa makalavati pamoja na ujenzi wa njia za mchepuo.
Naye Mbunge wa Iringa Mjini, Fadhili Ngajilo amesema wananchi wa Iringa wameupokea mradi huo kwa matumaini makubwa kutokana na mchango wake katika kuboresha usafiri na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika mji huo.


