Na John Bukuku, Dar es Salaam
Kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, katika Mkutano wa Uvumbuzi wa Nishati ya Nyuklia Afrika (NEISA 2026) uliofanyika Kigali nchini Rwanda, Amepaza sauti na kufungua ukurasa mpya katika safari ya Afrika kuelekea matumizi ya teknolojia ya nyuklia kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Katika kipindi ambacho mataifa mengi ya Afrika bado yapo kwenye mijadala ya sera na matarajio, Tanzania imeanza kuonesha ishara za kuingia kwenye hatua za utekelezaji wa vitendo.
Rais Samia ameendelea kujijengea taswira ya kiongozi mwenye maono mapana katika sekta ya nishati, hususan kupitia msukumo wake kwenye nishati safi ya kupikia, nishati jadidifu na sasa mjadala wa nishati ya nyuklia. Hotuba yake mjini Kigali haikuwa ya kawaida. Ilikuwa ni kauli ya kisera iliyobeba ujumbe wa kuhimiza Afrika kuacha kutegemea ahadi, maandiko na makongamano pekee, bali kuanza kuwekeza kwenye mifumo halisi ya utekelezaji wa teknolojia za kisasa za nishati.
Kauli yake kwamba “Afrika lazima itoke kwenye matarajio kwenda kwenye utekelezaji” ilionesha wazi kuwa changamoto ya nishati Afrika haiwezi kuendelea kujadiliwa kwa mtindo wa kusubiri misaada au maamuzi ya mataifa makubwa. Bara la Afrika linahitaji mifumo imara ya nishati itakayoweza kuhimili kasi ya ukuaji wa viwanda, teknolojia, usafiri wa kisasa, uchimbaji madini na ongezeko la matumizi ya kidijitali.
Kwa miaka mingi, mjadala wa nishati ya nyuklia barani Afrika ulikuwa ukiambatana na hofu kuhusu gharama, usalama na ukosefu wa wataalamu. Lakini sasa dunia imeanza kubadilika kutokana na ujio wa teknolojia mpya za Small Modular Reactors (SMRs) na Micro Modular Reactors (MMRs), ambazo ni rahisi zaidi kusimamia, salama na zenye gharama nafuu kwa nchi zinazoendelea.
Katika mazingira hayo, Tanzania imeanza kuonesha utayari wa kisera na kitaasisi kuingia kwenye safari ya muda mrefu ya matumizi ya teknolojia ya nyuklia. Kauli ya Rais Samia kwamba Tanzania inaendelea kutathmini matumizi ya nyuklia kama sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa kuongeza vyanzo vya nishati ni ishara kuwa serikali imeanza kuona nyuklia kama sehemu ya mustakabali wa uchumi wa taifa.
Kwa hakika, msimamo huo unaendana moja kwa moja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ambayo tayari imeitambua nyuklia kama moja ya vyanzo vinavyotarajiwa kusaidia ukuaji wa uchumi na upatikanaji wa nishati ya uhakika nchini. Hii ina maana kuwa mjadala wa nyuklia umeondoka kwenye ngazi za kitaalamu pekee na sasa umeingia rasmi kwenye mipango ya maendeleo ya taifa.
Kilichoipa uzito zaidi nafasi ya Tanzania katika mkutano huo ni namna ujumbe wa Tanzania ulivyoundwa. Mbali na Rais Samia, ujumbe huo ulimjumuisha Waziri wa Nishati, Deogratius John Ndejembi, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati anayeshughulikia masuala ya Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Felchesmi Mramba, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania, Prof. Najat Kassim Mohammed pamoja na viongozi wengine.
Uwepo wa ujumbe wa viongozi hao waloongozana na Rais katika mkutano huo ulikuwa ishara ya wazi kuwa Tanzania haikuenda Kigali kwa ajili ya kusikiliza hotuba pekee, bali kuonesha kuwa tayari imeanza safari ya utekelezaji wa mpango wa nyuklia.
Katika utekelezaji wa sera hiyo, Waziri Ndejembi ameanza kuonesha namna Tanzania ilivyojipanga kuingia kwenye zama mpya za teknolojia ya nyuklia kwa utaratibu wa kimataifa unaotambuliwa na International Atomic Energy Agency.
Kupitia Wizara ya Nishati, Tanzania tayari imeandaa Mpango wa Taifa wa Miaka Saba wa maendeleo ya nishati ya nyuklia unaozingatia mfumo wa hatua wa IAEA maarufu kama Milestones Approach. Hatua hiyo ni muhimu kwa sababu inaweka ramani ya taifa kuhusu namna ya kuingia kwenye matumizi ya nyuklia kwa uzalishaji wa umeme kwa usalama na ufanisi.
Serikali pia tayari imeandaa Waraka wa Baraza la Mawaziri unaoeleza mahitaji ya rasilimali, maandalizi ya kitaasisi pamoja na uwezo wa Tanzania kuanza matumizi ya nishati ya nyuklia kwa uzalishaji wa umeme. Hatua hii inaonesha kuwa mjadala wa nyuklia sasa umeingia kwenye ngazi za juu za maamuzi ya serikali.
Moja ya hatua kubwa zaidi zilizochukuliwa ni kuanzishwa kwa Taasisi ya Kitaifa ya Utekelezaji wa Nishati ya Nyuklia (NEPIO) tarehe 12 Novemba 2025. Taasisi hiyo ndiyo itakayoratibu maandalizi yote ya utekelezaji wa mpango wa taifa wa nyuklia kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za serikali.
Sambamba na hilo, Serikali imeunda Kamati ya Kitaifa ya Uongozi inayojumuisha makatibu wakuu na wakurugenzi wakuu wa wizara na taasisi mbalimbali pamoja na Technical Working Group kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa maandalizi ya nyuklia nchini. Hii inaonesha kuwa Tanzania imeamua kutumia mfumo wa kitaifa badala ya kuacha jukumu hilo kwa taasisi moja pekee.
Katika kuonesha namna Tanzania ilivyojipanga, ujumbe maalum wa International Atomic Energy Agency ulitembelea Tanzania mwezi Februari 2026 na kuridhishwa na maendeleo ya awali ya maandalizi ya utekelezaji wa mpango wa nyuklia. Hatua hiyo imeipa Tanzania uhalali mkubwa katika safari yake ya kuingia kwenye matumizi ya teknolojia ya nyuklia.
Serikali pia ipo katika hatua za kufanya maboresho ya sheria na mifumo ya udhibiti ikiwemo kuanzishwa kwa Mamlaka Huru ya Udhibiti wa Nishati ya Nyuklia (INRA). Hii ni hatua muhimu kwa sababu teknolojia ya nyuklia inahitaji mifumo madhubuti ya usimamizi, usalama na uwajibikaji wa kitaasisi.
Kwa mujibu wa Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania chini ya Prof. Najat Kassim Mohammed, Tanzania imeanza kuionesha Afrika kuwa ipo tayari kushiriki kikamilifu katika mapinduzi mapya ya teknolojia ya nyuklia. TAEC imeendelea kujenga uwezo wa kitaalamu, kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kushiriki kwenye mijadala ya kimataifa kuhusu matumizi ya amani ya teknolojia ya nyuklia.
TAEC pia imeanza tafiti za awali za upembuzi yakinifu kwa ajili ya maeneo yanayoweza kutumika kuzalisha umeme wa nyuklia. Tayari maeneo ya Misungwi mkoani Mwanza na Pangani mkoani Tanga yametambuliwa kutokana na vigezo vya kijiolojia, upatikanaji wa maji, idadi ndogo ya watu na uwepo wa miundombinu ya kusafirisha umeme kwenye gridi ya taifa.
Katika upande wa afya, Mkurugenzi wa Huduma za Kinga wa Taasisi ya Saratani Ocean Road, Dkt. Crispin Kahesa, ameonesha kuwa teknolojia ya nyuklia tayari imeanza kuleta mapinduzi makubwa katika huduma za saratani nchini Tanzania.
Kupitia huduma za Nuclear Medicine zinazotumia Gamma Camera, ORCI tayari inafanya uchunguzi wa kisasa wa mifupa, figo, tezi ya thyroid pamoja na vipimo vingine vya kitabibu. Aidha, taasisi hiyo inatoa huduma za Radioactive Iodine kwa wagonjwa wa saratani ya tezi pamoja na Radiotherapy kwa matibabu ya saratani mbalimbali.
Serikali imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika huduma hizo kupitia mradi wa PET-CT Scan na Cyclotron wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 18.9. Teknolojia hiyo itawezesha Tanzania kugundua saratani mapema zaidi, kufuatilia usambaaji wa ugonjwa mwilini na kupima mwitikio wa matibabu kwa usahihi mkubwa.
Kupitia Cyclotron, Tanzania sasa itaweza kuzalisha dawa za mionzi hapa nchini badala ya kutegemea kuagiza kutoka nje. Hii ni hatua kubwa itakayopunguza gharama za matibabu na kuongeza upatikanaji wa huduma kwa wananchi wengi zaidi.
Mbali na hilo, Serikali imenunua mashine mpya tatu za Radiotherapy zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni saba, hatua ambayo itaifanya ORCI kuwa na mashine tano za kisasa za tiba ya mionzi. Uwekezaji huu unaonesha wazi kuwa Tanzania tayari imeanza kutumia teknolojia ya nyuklia katika kuboresha huduma za afya kwa kiwango kikubwa.
Tanzania pia imeendelea kuwekeza katika mafunzo ya wataalamu wa Oncology, Nuclear Medicine, Medical Physics na Radiography ili kuhakikisha uwepo wa wataalamu wa kutosha watakaoweza kuendesha teknolojia hizi kwa usalama na ufanisi mkubwa.
Kwa ujumla, mkutano wa Kigali umeonesha jambo moja muhimu: Tanzania haipo tena kwenye hatua ya kuzungumzia nyuklia kama ndoto ya baadaye, bali imeanza kujenga mifumo ya utekelezaji wa kweli. Kupitia uongozi wa Rais Samia, usimamizi wa Waziri Ndejembi, maandalizi ya TAEC chini ya Prof. Najat Kassim Mohammed pamoja na uwekezaji mkubwa wa ORCI katika afya, Tanzania inaanza kujijengea nafasi ya kuwa moja ya nchi zitakazoongoza matumizi ya amani ya teknolojia ya nyuklia katika Afrika Mashariki na Kati.
Katika dunia inayokwenda kwa kasi kwenye mapinduzi ya teknolojia, viwanda na ushindani wa kiuchumi, mataifa yatakayochelewa kuwekeza kwenye usalama wa nishati yanaweza kubaki nyuma. Na huenda historia ikaukumbuka mkutano wa Kigali kama sehemu ambayo Afrika ilianza rasmi safari yake ya kutoka kwenye ahadi za nishati kwenda kwenye utekelezaji wa kweli.
MAONI/ USHAURI- 0627869841- 0713410676
