Baadhi ya wakulima wanaohudumiwa na Chama kikuu cha ushirika wilaya ya Tunduru(TAMCU LTD)wakifuatilia mwendendo wa mnada wa kwanza wa zao la ufuta uliofanyika jana mjini Tunduru(Picha na Muhidin Amri)

Afisa biashara mwandamizi wa soko la bidhaa Tanzania(TMX)Mohmaed Nyasama kushoto, akimuonyesha Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Denis Masanja katikati, bei ya zao a ufuta kwenye mnada wa kwanza uliofanyika jana kulia mwenyekiti wa Chama kikuu cha ushirika wilayani Tunduru Tamcu Ltd Mussa Manjaule(Picha na Muhidin Amri)

Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Denis Masanja, akiuzungumza na wakulima,wafanyabiashara na wawakilishi wa taasisi za fedha wakati wa mnada wa kwanza wa zao la ufuta uliofanyika jana ambapo jumla ya kilo 994,618 wenye thamani ya Sh.bilioni 2.4 umeuzwa (Picha na Muhidin Amri).

Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma Denis Masanja kushoto, Mwenyekiti wa Chama kikuu cha ushirika wilayani humo Tamcu Mussa Manjaule katikati na baadhi ya wafanyakazi wa Tamcu wakifuatilia mwendendo wa bei ya zao la ufuta kwenye mnada wa kwanza uliofanyika jana(Picha na Muhidin Amri).

 Mwenyekiti wa Chama kikuu cha ushirika wilaya ya Tunduru(Tamcu Ltd)Mussa Manjaule,akizungumza na wakulima wa zao la ufuta waliofika kwenye mnada wa kwanza uliofanyika jana katika ofisi ya Mkuu wa wilaya Denis Masanja katikati na kushoto Katibu Tawala wa wilaya hiyo Milongo Sanga.

………….

Na Mwandishi Wetu, Tunduru

CHAMA kikuu cha ushirika wilayani Tunduru(TAMCU LTD) Mkoani Ruvuma,kimeuza kilo 994,681 za ufuta  wa wakulima wenye thamani ya Sh.2,463,668,786 wanaohudumiwa na Chama hicho katika mnada wa kwanza kupitia mfumo wa soko la bidhaa Tanzania(TMX).

Kaimu meneja wa Tamcu Zainabu Sedema alisema, katika mnada huo bei ya  chini ilikuwa Sh.2,410,bei ya juu Sh.2,520 na bei wastani Sh.2,477 na Tamcu itafanya malipo kwa wakulima kwa kushirikiana na maafisa ushirika wenye dhamana ya kuhakikisha vyama vya msingi vya ushirika vinaandaa taarifa sahihi za wakulima kwa ajili ya kufanyiwa malipo.

“Pamoja na kituo cha malipo ya pamoja(Payment Center),hata hivyo Tamcu Ltd ina kituo cha kuchapa majina ya wakulima waliopo kila Amcos ili kujiridhisha na taarifa zao kabla ya malipo hayo”alisema Sendema.

Kwa mujibu wa Sendema,katika msimu 2025/2026 Chama kikuu kiliuza kilo 5,042,260 zenye thamani ya Sh.bilioni 12,185,051,130 kupitia minada sita na mnada wa kwanza  uliofanyika katika kijiji cha Mchesi tarafa ya Lukumbule ambapo kilo 1,273,487.0 ziliuzwa kwa bei ya wastani ya Sh.2,439 kwa kilo moja.

Mwenyekiti wa Tamcu Mussa Manjaule,amewapongeza wakulima waliohudhuria mnada huo kukubali kuuza ufuta kwa bei iliyoletwa na wanunuzi katika mnada wa kwanza kwa msimu wa mauzo 2026/2027.

“niwakumbushe ndugu zangu mnada wa kwanza msimu 2025/2026 bei ilikuwa Sh.2439 leo tumeanza mnada wetu wa kwanza msimu 2026/2027 bei imekuwa nzuri Sh.2,477 kwa hiyo kuna tofauti ya Sh.38  hivyo tunapiga hatua kubwa”alisema Manjaule.

Manjule alisema,Chama kikuu cha ushirika wamejipanga kuhakikisha wanalipa fedha kwa wakati na hakuna mkulima yoyote atakayekosa fedha baada ya kufikisha ufuta kwenye maghala ya  vyama vya msingi vya ushirika.

Mkuu wa wilaya ya Tunduru Denis Masanja,amekitaka Tamcu kuhakikisha wakulima wanalipwa fedha kwa wakati ndani ya muda wa siku tatu baada ya mnada kufanyika.

Ameziomba taasisi za fedha hususani benki kuamsha akaunti za wakulima  ili kuepusha usumbufu unaoweza kusababisha baadhi ya wakulima kuchelewa kuingiziwa fedha zao.

Masanja, ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya usalama ya wilaya Tunduru,amepongeza mfumo wa uuzaji wa mazao ya wakulima kupitia soko la bidhaa Tanzania(TMX)ambao umesaidia  sana kupunguza hasara,udanganyifu ,ulinzi wa mzao na kipato halisi kwa wakulima.

Amewataka wakulima, kuendelea kutumia mfumo  wa stakabadhi ghalani katika kuuza mazao yao na kuacha kuuza mazao kwa njia ya magendo ambao umekuwa chanzo cha kuwarudisha nyuma licha ya juhudi kubwa wanazofanya mashambani.

“Wkulima nawapa habari njema,Serikali kwa kuwapenda wakulima imeongeza mazao ya njugu,kunde na karanga kwenye mfumo wa stakabadhi ghalani,kwa hiyo tunategemea wananchi wa wilaya ya Tunduru wataanza kufaidika na mpango huo”alisema Masanja.

Akizungumza kwa niaba ya wakulima Juma Bakari alisema,wameridhika na bei iliyotoletwa na wanunuzi kwani hawakutegemea kupata bei hiyo kutokana na hali ya hewa hasa vita vinavyoendelea kwa baadhi ya nchi Duniani,hivyo ameomba minada inayofuata bei isishuke ili kuwapa matumaini wakulima waweze kuendelea na uzalishaji wa zao hilo.