Maadhimisho ya Kwanza ya Siku ya Ziwa Victoria yamefanyika katika Viwanja vya Nyamhongolo jijini Mwanza yakiweka historia mpya kwa ukanda wa Afrika Mashariki, yakisisitiza mshikamano, usalama na usimamizi endelevu wa rasilimali za Ziwa Victoria linalowategemeza mamilioni ya wananchi katika sekta za uchumi, uvuvi na usafirishaji.
Akizungumza katika kilele cha maadhimisho hayo Mgeni rasmi Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Mwigulu Nchemba, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhakikisha Ziwa Victoria linalindwa dhidi ya changamoto za ujangili, uhalifu na uharamia majini, ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kufanya shughuli zao katika mazingira ya amani na usalama.
Amesema Ziwa Victoria ni rasilimali ya kimkakati inayowaunganisha Tanzania, Kenya na Uganda, huku Rwanda na Burundi nazo zikiendelea kuwa wadau muhimu wa Bonde hilo, hivyo mshikamano wa kikanda unabaki kuwa msingi muhimu wa maendeleo endelevu ya ukanda mzima.
Waziri Mkuu amesisitiza kuwa kauli mbiu ya mwaka huu isemayo “Maji Yetu, Mustakabali Wetu: Tuungane kwa Usimamizi Endelevu wa Bonde la Ziwa Victoria” inapaswa kutafsiriwa katika vitendo kupitia ulinzi wa mazingira, kuimarisha usalama majini na kuhakikisha matumizi endelevu ya rasilimali hiyo kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki James Millya, amesema maadhimisho hayo yamefungua ukurasa mpya wa mshikamano wa kikanda, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na nchi wanachama kuhakikisha Ziwa Victoria linakuwa injini ya maendeleo endelevu ya wananchi wa ukanda huo.
Maadhimisho hayo yamehitimishwa kwa kutangazwa rasmi kwa Siku ya Ziwa Victoria, ambayo sasa itaadhimishwa kila mwaka tarehe 21 Mei, ikiwa ni hatua muhimu ya kuimarisha mshikamano wa kikanda na kulinda bonde la ziwa hilo kwa mustakabali wa vizazi vijavyo.

