Na Mwamvua Mwinyi
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete amesema serikali itaendelea kuboresha maslahi ya watumishi wa umma nchini kadri bajeti itakavyoruhusu.
Ridhiwani ameyasema hayo wakati akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano wa 13 wa Chama cha Waandishi Waendesha Ofisi Tanzania (TAPSEA) uliofanyika Ngurdoto mkoani Arusha.
Mkutano huo ulifunguliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Emanuel Nchimbi na kuwashirikisha wanachama takriban 5,050 kutoka Serikali Kuu, Serikali za Mitaa pamoja na taasisi mbalimbali za Tanzania Bara na Zanzibar.
Akizungumza katika mkutano huo, Dk. Nchimbi aliwataka wajumbe watakaoshiriki uchaguzi wa viongozi wapya wa chama hicho kuzingatia haki, umoja na kuepuka vitendo vinavyoweza kukipotezea mwelekeo chama .
Kwa upande wake, Ridhiwani alisema serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha mazingira na maslahi ya watumishi wa umma, ikiwemo kupandisha madaraja, kubadili miundo na vyeo pamoja na kulipa madeni ya mishahara.
Alisema serikali itaendelea kutekeleza maboresho hayo katika bajeti ya mwaka huu na miaka ijayo kulingana na upatikanaji wa fedha.
“Serikali itaendelea kuhakikisha watumishi wa umma wananeemeka na matunda ya serikali yao kupitia maboresho mbalimbali ya kiutumishi,” alisema Ridhiwani

