Na Farida Mangube, Morogoro 

Jamii imetakiwa kuendelea kuwajali watoto wenye mahitaji maalum na wanaoishi katika mazingira magumu kwa kuwapa upendo, msaada na ukaribu ili kuwajengea matumaini ya maisha bora.

Wito huo umetolewa leo, Mei 21, 2026, na Afisa Ushirika wa Wilaya ya Mvomero, Aidan Emily Nyamweru, wakati wa ziara ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika Wilaya ya Mvomero katika Kituo cha Kulelea Watoto Wenye Mahitaji Maalum cha Amani, ambapo walifanya matendo ya huruma ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Jukwaa la Ushirika la Wilaya pamoja na maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani.

Katika ziara hiyo, tume hiyo imekabidhi mifuko miwili ya unga, sukari, daftari, rimu na kalamu kwa ajili ya watoto wa kituo hicho.

Afisa Ushirika huyo amesema kuwa kabla ya kufanyika kwa jukwaa la ushirika wilaya, wamekuwa na utaratibu wa kurejesha kwa jamii kupitia matendo ya huruma ili wananchi waelewe mchango wa ushirika katika jamii.

Amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa msingi wa saba wa ushirika unaosisitiza umuhimu wa kujali jamii.

Kwa upande wake, Mwalimu wa Shule ya Msingi Amani Mvomero, Athuman Shambani, ameushukuru Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa msaada huo huku akiomba wadau wengine kuendelea kusaidia vituo vya kulelea watoto yatima na wenye mahitaji maalum.

“Watoto hawa wanahitaji ukaribu, upendo na msaada kutoka kwa jamii ili wajione kuwa ni sehemu ya jamii,” alisema Athuman.