Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Azzan Zungu amesema viongozi wa Wizara ya Ujenzi wanafanya kazi kubwa na nzuri katika utekelezaji wa majukumu yao.
Akizungumza mara baada ya Bunge kupitisha bajeti hiyo jijini Dodoma, Spika Zungu amempongeza Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, Naibu Waziri Mhandisi Godfrey Kasekenya, Katibu Mkuu pamoja na wataalamu wote wa Wizara hiyo wakiwemo wataalamu wa TANROADS na taasisi nyingine zilizo chini ya Wizara kwa kazi nzuri wanayoifanya katika sekta ya miundombinu nchini.
“Mambo hapa bungeni yamekwenda kwa uhalisia na hoja, na Serikali imejibu kwa hoja. Wabunge na wananchi wameridhika,” alisema Spika Zungu.
Mapema jana Mei 20, 2026 Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega aliwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2026/2027 ambapo imeomba kuidhinishiwa jumla ya Shilingi 2,564,441,414,000 kwa ajili ya matumizi ya kawaida pamoja na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Akiwasilisha bajeti hiyo, Waziri Ulega alisema kuwa fedha hizo zinalenga kuimarisha utekelezaji wa miradi ya miundombinu nchini hususan katika sekta ya barabara ili kuongeza ufanisi wa usafirishaji na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Kwa mujibu wa makadirio hayo, kati ya fedha zilizoombwa, Shilingi 97,104,935,000 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya Wizara na taasisi zake, huku Shilingi 2,467,336,479,000 zikielekezwa katika miradi ya maendeleo.
Aidha, kati ya fedha za matumizi ya kawaida, Shilingi 92,209,218,000 ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi na Shilingi 4,895,717,000 zimetengwa kwa matumizi mengineyo ya uendeshaji wa shughuli za kila siku.
Kwa upande wa bajeti ya maendeleo, fedha za ndani zimepangwa kuwa Shilingi 1,544,872,147,000 huku fedha za nje zikiwa Shilingi 922,464,332,000. Fedha za ndani zinajumuisha Shilingi 1,047,405,500,000 kutoka Mfuko wa Barabara pamoja na Shilingi 497,466,647,000 kutoka Mfuko Mkuu wa Serikali.
Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi imeeleza kuwa fedha hizo zitatumika katika ujenzi, ukarabati na uboreshaji wa miundombinu ya barabara nchini kwa lengo la kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa pamoja na kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi nchini.
