Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Patrobas Katambi, amekutana na kufanya mazungumzo na mwakilishi wa Shirika la Kimataifa la Watoto Duniani (UNICEF), Bi. Elke Wisch, kuhusu kuimarisha ushirikiano katika masuala ya ulinzi na ustawi wa watoto nchini.

‎Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Katambi amesema kuwa, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inaendelea kushirikiana kwa karibu na UNICEF katika utekelezaji wa miradi mbalimbali inayolenga ustawi na ulinzi wa watoto kupitia Jeshi la Polisi pamoja na Jeshi la Magereza.

‎Waziri Katambi amesema, kwa upande wa Jeshi la Polisi, tayari hatua mbalimbali zimechukuliwa ikiwemo kuanzishwa kwa madawati ya jinsia na watoto pamoja na miongozo yenye lengo la kuwapatia watoto na waathirika wa ukatili huduma za kisheria na ulinzi dhidi ya vitendo vya unyanyasaji na migogoro ya kisheria.

‎Aidha, Waziri Katambi amesema ushirikiano huo umewezesha utoaji wa mafunzo kwa maafisa wa polisi kuhusu namna ya kuzuia na kushughulikia vitendo vya ukatili wa kijinsia, unyanyasaji wa watoto pamoja na uhalifu wa mtandaoni unaowaathiri watoto na makundi mengine yaliyo hatarini.

‎Vilevile, ameipongeza UNICEF kwa mchango wake mkubwa katika kushirikiana na Jeshi la Magereza kuhakikisha watoto waliopo magerezani wanapata ulinzi, malezi na huduma stahiki kwa mujibu wa sheria na haki za mtoto.

‎Pamoja na mambo mengine, Waziri Katambi amesema ushirikiano kati ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na UNICEF utaandaa programu zitakazofundisha watoto jinsi ya kukabiliana na majanga mbalimbali yakiwemo mafuriko, moto na dharura zingine na kufanya kampeni ya usalama na unyanyasaji

‎Kwa upande wake, Bi. Elke Wisch amesema UNICEF itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ili kuhakikisha watoto wanapata mazingira salama ya kuishi, kujifunza na kukua bila vitisho vya ukatili na unyanyasaji.

‎Amesema shirika hilo linaipa kipaumbele agenda ya ulinzi wa mtoto, hususan katika kukabiliana na changamoto za ukatili wa kijinsia, ajira za watoto, ndoa za utotoni pamoja na matumizi yasiyo salama ya mitandao kwa watoto na vijana.

‎Mkutano huo umehudhuriwa na baadhi ya viongozi na maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, UNICEF pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama.

‎Kikao hicho kimefanyika Makao Makuu ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, jijini Dodoma, Mei 21, 2026.