📍Mwanza
WAKAGUZI wa Migodi na Baruti nchini wametakiwa kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao na kuimarisha usimamizi wa usalama migodini ili kudhibiti ajali, kulinda maisha ya wafanyakazi, mazingira na rasilimali za Taifa.
Kauli hiyo imetolewa jijini Mwanza na Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet Lekashingo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Tano wa Mwaka wa Wakaguzi wa Migodi na Baruti.
Dkt. Lekashingo amesema wakaguzi hao wana nafasi muhimu katika kuhakikisha shughuli za uchimbaji wa madini zinafanyika kwa usalama, ufanisi na kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.
Amesema shughuli za uchimbaji madini ni miongoni mwa kazi zenye hatari kubwa hivyo zinahitaji usimamizi madhubuti ili kuhakikisha uchimbaji endelevu unafanyika bila kuhatarisha maisha ya watu na mazingira.
Katika hatua nyingine, Dkt. Lekashingo amepongeza viongozi na watumishi wa Tume ya Madini kwa kuvuka lengo la makusanyo ya mwaka wa fedha 2025/2026 kabla ya muda.
Amesema lengo la makusanyo kwa mwaka huo lilikuwa Shilingi trilioni 1.2, huku hadi Mei 18, 2026 makusanyo yakifikia Shilingi trilioni 1.203 sawa na asilimia 100.31 ya lengo lililowekwa.
“Mafanikio haya ni uthibitisho wa usimamizi madhubuti, uwajibikaji, uzalendo na juhudi kubwa mnazozifanya katika kusimamia Sekta ya Madini,” amesema Dkt. Lekashingo.
Aidha, amesema Serikali kupitia Tume ya Madini itaendelea kuboresha mazingira na vitendea kazi kwa wakaguzi wa migodi na baruti ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Akimwakilisha Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo, Mkurugenzi wa Leseni wa Tume, Eng. Aziza Swedi, amewataka wakaguzi wa migodi kuwa wabunifu na kutumia taaluma zao ipasavyo katika kusimamia ukaguzi wa migodi nchini.
Eng. Swedi amesema ni muhimu kwa wakaguzi hao kujiendeleza kitaaluma ili kwenda sambamba na kasi ya mabadiliko ya teknolojia pamoja na matumizi ya mbinu za kisasa za ukaguzi migodini.
Pia amesisitiza umuhimu wa kuzingatia maadili ya kazi na kutoa huduma kwa haki bila kuwaonea wadau wa sekta ya madini.
“Mkaguzi yeyote atakayesababisha sifa hii kuharibika, hatua kali za kimaadili zitachukuliwa dhidi yake na uteuzi wake kufutwa mara moja,” amesema Eng. Swedi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira, Eng. Hamisi Kamando, amesema idara hiyo ina jukumu la kuhakikisha shughuli za uchimbaji madini zinafanyika kwa kuanzia hatua za awali za uendeshaji wa mgodi hadi kufungwa kwake.
Amesema idara hiyo pia inasimamia usalama, afya, mazingira pamoja na utekelezaji wa sheria na taratibu zote za uchimbaji ili kuhakikisha migodi inaleta manufaa kwa Taifa bila kuathiri mazingira na jamii zinazozunguka maeneo ya uchimbaji.

