Na Silivia Amandius.

Kagera.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kagera imesema imefanikiwa kurejesha zaidi ya Shilingi milioni 624 kutokana na kesi mbalimbali za rushwa zilizoshindwa mahakamani katika kipindi cha Julai 2025 hadi Mei 2026. Mafanikio hayo yametajwa kuwa sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo kwa kipindi cha Januari hadi Machi mwaka 2026.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Naibu mkuu wa takukuru Leonard Swai leo May 21, mwaka huu kwa waandishi wa habari katika ofisi za takukuru amesema TAKUKURU Mkoa wa Kagera ilifungua kesi 61 mahakamani ambapo mashauri 52 yaliamriwa na kati ya hayo, mashauri 50 sawa na asilimia 97 yalishindwa na upande wa watuhumiwa huku mashauri mawili sawa na asilimia 3 yakishindwa na upande wa Jamhuri. Mashauri mengine tisa bado yanaendelea mahakamani. Kupitia ushindi huo, taasisi hiyo imefanikiwa kurejesha kiasi cha Shilingi 624,612,385.

Aidha, TAKUKURU imeeleza kuwa katika kipindi hicho ilipokea taarifa 132 ambapo taarifa 83 zilihusu vitendo vya rushwa na taarifa 49 hazikuhusu rushwa. Taarifa zilizohusu rushwa zilifanyiwa uchunguzi na kusababisha kufunguliwa kwa majalada 12 ya kesi mahakamani huku uchunguzi mwingine ukiendelea. Vilevile, TAKUKURU Wilaya ya Kyerwa ilifanikiwa kurejesha Shilingi milioni 30 zilizokuwa zimetolewa kwa kikundi cha wanawake wafugaji nyuki wa Kata ya Katera baada ya kubainika fedha hizo kutumika kinyume na taratibu.

Katika hatua nyingine, TAKUKURU Wilaya ya Ngara ilidhibiti ujenzi chini ya kiwango wa zahanati ya Kijiji cha Runzenze, Kata ya Ntobeye, baada ya uchunguzi kubaini udhaifu katika msingi wa jengo uliosababishwa na mchanganyiko hafifu wa zege. Sambamba na hilo, taasisi hiyo ilifuatilia matumizi ya zaidi ya Shilingi bilioni 2.2 katika utekelezaji wa miradi 29 ya maendeleo na kutoa ushauri wa maboresho ili kuhakikisha thamani ya fedha za umma inalindwa.

Pia TAKUKURU Mkoa wa Kagera imeendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu madhara ya rushwa ambapo imefanikiwa kufanya semina 22, mikutano ya hadhara pamoja na kuimarisha klabu 99 za wapinga rushwa katika shule na jamii, hatua ambayo imechangia kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu wajibu wao katika kupinga vitendo vya rushwa.

TAKUKURU imetoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na taasisi hiyo kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa mali za umma ili kusaidia kujenga jamii yenye uwajibikaji, uadilifu na maendeleo ya kweli kwa manufaa ya taifa na vizazi vijavyo.