Kuanzishwa kwa Klabu za Maadili katika shule za msingi na sekondari wilayani Hanang mkoani Manyara kumetajwa kuwa moja ya sababu za mabadiliko kinidhamu na ukuaji wa taaluma miongozi mwa wanafunzi wilayani humo.

Hayo yamesemwa kwa nyakati tofauti na viongozi, walimu na wanafunzi wa shule zenye Klabu za Maadili wilayani humo wakati wa zoezi la kutembelea wanachama wa klabu hizo lililofanyika kuanzia tarehe 18 hadi 20 Mei, 2026 na kuratibiwa na Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Kaskazini-Arusha.

Akizungumzia uwepo wa klabu hizo Afisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Wilaya ya Hanang Bi. Sophia Msoffe amesema klabu za maadilli zimekua chanzo katika kujenga maadili na hali ya kujiamini kwa wanafunzi hasa katika kujieleza au kuchangia jambo lolote la kitaaluma.

“Klabu hizi zimekua zikifanyika katika mazingira huru ambapo watoto wanakua na nafasi ya kuonyesha walichonacho na pia kupokea kwa undani kile wanachopata kutoka kwa walimu walezi wa klabu na wakufunzi kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma,” alisema Bi. Sophia.

Kwa upande wake mkuu wa shule ya sekondari Measkron Bw. Seluwin Mkisi amesema licha ya klabu hizo kuwa nyenzo muhimu katika kukuza taaluma na uadilifu pia imesaidia kuwajenga kiroho wanafunzi na kupelekea kuwa na tabia njema.

“Licha ya kusaidia upande wa taaluma, lakini uwepo wa klabu hii umesaidia kuwajenga watoto wetu kiroho, kwa sababu tunapoongelea maadili ni pamoja na muonekano ambao upelekea tabia njema na hatimaye kupata watoto waadilifu kimwili na kiroho pia,” alisema mwalimu Mkisi.

Nae mwalimu mlezi wa Klabu ya Maadili shule ya msingi Jorodom Bi. Rose Manda amesema kuwa uwepo wa klabu ya maadili shuleni hapo umechangia katika kupunguza utoro na kurekebisha nidhamu kwa wanafunzi hasa kupitia kazi mbali mbali wanazofanya katika klabu yao.

“Klabu ya maadili imechangia kurekebisha nidhamu na kupunguza utoro kwa kiasi kikubwa hapa shuleni, huku wanafunzi ambao sio wanachama wakijitaidi kuwa na nidhamu nzuri na kuhudhuria shule bila kukosa kwa kuamini kuwa ipo siku watapata nafasi ya kuwa wanachama wa klabu ya maadili,” alisema mwalimu huyo.

Kwa upande wake mwanafunzi wa sekondari ya Wasichana Nangwa, Sharifa Saidi amesema uwepo wa Klabu ya Maadili umesaidia wao kuwa na maadili mazuri ndani na nje ya shule kwa kuwa watiifu na kuheshimu wazazi na watu wengine kwa kuyafanya yale wanayofundishwa kwenye klabu yao.

Mradi wa Klabu za Maadili kwa shule za msingi, sekondari na vyuo umekua ukiratibiwa na Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambapo kupitia mradi huo wanachama wa klabu hizo wamekua wakifanya shughuli mbali mbali kama vile kupanda miti, kutengeneza bustani za maua na mboga mboga pamoja na sanaa za maigizo kwa lengo la kukuza taaluma na kuwajenga kimaadili na uzalendo angali wakiwa wanafunzi.