Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. James Kinyasi Millya (Mb.), ametembelea Kampuni ya Huduma za Meli Tanzania (TASHIKO) na meli ya MV Mwanza ,jijini Mwanza kujionea namna shughuli za usafiri wa majini zinavyoendeshwa na mchango wake katika kukuza uchumi na ushirikiano wa kikanda.
Katika ziara hiyo, Mhe. Millya aliambatana na Naibu Katibu Mkuu Balozi Saidi Shaibu Mussa pamoja na Mkurugenzi wa Uchumi, Miundombinu na Huduma za Jamii, Mhandisi Abdillah Mataka, ambapo walipokelewa na Mkurugenzi Mtendaji wa TASHIKO, Bw. Eric Benedict Hamissi pamoja na menejimenti ya kampuni hiyo.
Akitoa maelezo kuhusu shughuli za TASHIKO, Bw. Hamissi alisema kampuni hiyo ina mchango mkubwa katika kuunganisha Tanzania na mataifa jirani kupitia huduma za usafiri wa majini, huku akieleza kuwa uwepo wa meli mpya ya MV Mwanza umeongeza hadhi na uwezo wa usafiri katika ukanda wa Maziwa Makuu.
Kwa upande wake, Mhe. Millya amepongeza juhudi zinazofanywa na TASHIKO kuimarisha huduma za usafiri wa majini, akieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kufungua fursa za biashara, utalii na kuimarisha uhusiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na nchi jirani zinazozunguka Ziwa Victoria.
Aidha, amesema Wizara itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali kuhakikisha sekta ya usafiri wa majini inatumika kama nyenzo ya kukuza diplomasia ya uchumi na ushirikiano wa kikanda.

