MWENYEKITI wa Kitongoji cha Burunga wilayani Serengeti mkoani Mara, James Makuru, ameipongeza Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi kwa kuendelea kutoa kipaumbele katika utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Serengeti, huku akimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Sita wa kupeleka mradi huo mkubwa katika eneo la Burunga.
Akizungumza baada ya kusikia maelezo ya bajeti hiyo, Makuru amesema wananchi wa Burunga na Wilaya ya Serengeti kwa ujumla wanaishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa kujengwa kwa kiwanja hicho ambacho kitafungua fursa nyingi za maendeleo kwa wananchi.
“Hii ni fursa kubwa sana kwa wananchi wa Serengeti. Vijana wengi watapata ajira wakati wa ujenzi wa kiwanja hiki, lakini hata baada ya ujenzi kukamilika bado kutakuwa na nafasi nyingi za ajira hapa hapa kwenye uwanja wa ndege,” amesema James Makuru.
Amesema mbali na ajira, mradi huo utaongeza shughuli za biashara kutokana na ongezeko la watalii na wageni watakaokuwa wakitumia kiwanja hicho cha kimataifa kufika Serengeti.
“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuona Serengeti inastahili kuwa na International Airport. Huu ni mradi mkubwa wa maendeleo kwa wananchi wetu,” amesema.
Nao baadhi ya Wananchi wa kijiji cha Burunga wilayani Serengeti mkoani Mara wameipongeza Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi kwa uamuzi wa Serikali wa kuendelea na mradi wa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Serengeti, wakisema mradi huo ni chachu ya maendeleo na fursa mpya za kiuchumi kwa wananchi wa eneo hilo.
Miongoni mwa wananchi hao ni Steven Benjamin Ntumbo pamoja na mzee philipo manyanya ambapo wamesema wanayomfuraja kubwa sana kuona maandalizi ya ujenzi wa kiwanja hicho yanaendelea chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
“Sisi tuna furaha sana kuona uwanja wa ndege unaanza kujengwa hapa. Hii ni fursa kubwa kwa wananchi wa Serengeti na tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kufanya uamuzi huu mkubwa wa maendeleo,” amesema Ntumbo.
Wamesema eneo la Serengeti ni kitovu cha utalii hivyo uamuzi wa kujenga kiwanja hicho katika eneo hilo ni sahihi na utasaidia wananchi kunufaika moja kwa moja na rasilimali ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
“Hapa ndiyo kitovu cha utalii, kwa hiyo tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuona umuhimu wa kujenga uwanja huu. Utasaidia wananchi wa Serengeti kuona faida ya uwepo wa hifadhi yetu,” wamesema.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Uchukuzi kwa hatua ya kihistoria ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Serengeti, akisema mradi huo ni ukombozi mkubwa kwa sekta ya utalii na uchumi wa taifa kwa ujumla.
Amesema uamuzi huo ni matokeo ya maono ya muda mrefu ya wadau wa utalii, viongozi wa serikali pamoja na wananchi wa Mkoa wa Mara waliokuwa wakisisitiza umuhimu wa kuboreshwa kwa miundombinu ya usafiri katika eneo la Serengeti.
Mradi huo unatarajiwa kuongeza ukuaji wa sekta ya utalii nchini sambamba na kulinda mazingira ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kupitia mfumo wa “Green Airport” unaozingatia utunzaji wa mazingira
