DIWANI wa Kata ya Uwanja wa Ndege, Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Matoke Joseph Michael, amesema wananchi wa eneo hilo wamepokea kwa furaha Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi baada ya Serikali kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Serengeti, hatua inayotarajiwa kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi na kukuza sekta ya utalii.

Amesema mradi huo ni matokeo ya dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha miundombinu ya uchukuzi na kufungua fursa za maendeleo kwa wananchi.

Michael amesema uwanja huo ambao umekuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu sasa umeanza kutekelezwa, na utachochea ukuaji wa ajira, biashara na kuongeza mapato yatokanayo na sekta ya utalii katika Wilaya ya Serengeti.

Ameeleza kuwa uwanja huo utarahisisha usafiri wa watalii na kufanya Serengeti kuendelea kuwa moja ya maeneo muhimu ya kiuchumi duniani.

Pia amewapongeza wananchi waliotoa maeneo kwa ajili ya mradi huo pamoja na wataalamu wanaousimamia, akisisitiza kuwa ushirikiano wao umechochea mafanikio ya awali ya utekelezaji wake.

Aidha, ametoa wito kwa wananchi wa Serengeti kujiandaa kutumia fursa zitakazojitokeza kupitia mradi huo katika sekta za kilimo, biashara na huduma za utalii ili kunufaika moja kwa moja na uwekezaji huo mkubwa wa Serikali.

Naye mkazi wa Kijiji cha Burunga, Peter Mgaya Mwita, ameipongeza Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi kwa kuendelea kuipa kipaumbele miradi ya kimkakati, akisema itabadilisha kwa kiasi kikubwa uchumi wa Serengeti.

Amesema mradi huo sasa unaonyesha matumaini mapya chini ya Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, na utachochea ukuaji wa ajira, biashara na sekta ya utalii.

Mwita amesisitiza kuwa kukamilika kwa uwanja huo kutaleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kuwataka wananchi kujiandaa kikamilifu kutumia fursa zitakazojitokeza

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, Amesema uamuzi huo ni matokeo ya maono ya muda mrefu ya wadau wa utalii, viongozi wa serikali pamoja na wananchi wa Mkoa wa Mara waliokuwa wakisisitiza umuhimu wa kuwepo uwanja wa Ndege katika eneo la Serengeti.