WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo, amepokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Kuwait nchini Tanzania, Salem Yousif Alhamdan, katika kikao kifupi kilichofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.
Katika kikao hicho, viongozi hao walijadili masuala mbalimbali ya ushirikiano wa kidiplomasia na kuahidi kuendelea kuimarisha uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Kuwait kwa manufaa ya pande zote mbili, hususan katika sekta za uchumi, zikiwemo biashara, uwekezaji, miundombinu, afya, kilimo na maji.
Mhe. Kombo amempongeza Mheshimiwa Alhamdan kwa uteuzi wake na amemuhakikishia ushirikiano wakati wote atakapokuwa anahudumu hapa nchini
Naye Mhe. Alhamdan, ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano uliopo na kuahidi kuendeleza ushirikiano huo kupitia maeneo ya kipaumbele kwa manufaa ya wananchi wa pande zote.

