NAIBU Spika wa Bunge, Daniel Sillo, ametoa wito kwa wananchi na wadau mbalimbali kushiriki katika kuchangia huduma za matibabu ya upandikizaji Uloto kwa Watoto wenye ugonjwa wa Sicle Cell na upandikizaji figo kwa wenye uhitaji hapa nchini.
Amesema licha ya mafanikio yaliyopatikana ya huduma hizo za upandikizaji uloto na figo kutolewa hapa nchini na hivyo kuokoa fedha nyingi ambazo zingeweza kutumika endapo wananchi wangeenda kutibiwa nje ya nchi, bado gharama za utoaji wa huduma hizo ni kubwa na zinahitaji ushirikiano mpana kutoka kwa jamii.
Sillo aliyasema hayo wakati wa hafla ya chakula cha jioni iliyowakutanisha viongozi waandamizi wa mkoa wa Dodoma, wabunge na wadau mbalimbali kwa lengo la kujadili namna ya kuimarisha mfuko wa kusaidia matibabu ya upandikizaji uloto na figo pamoja na huduma nyingine za kibingwa.
Alisema kila mwananchi anapaswa kutambua kuwa kuchangia huduma hizo si jukumu la srrikali na taasisi pekee, bali ni wajibu wa pamoja kwa kuwa magonjwa kama ya figo na sikoseli hayachagui mtu kwa nafasi yake, dini wala hali ya maisha.
“Tunaposhiriki katika michango hii si kwa ajili ya taasisi moja, bali tunaunga mkono huduma za kitaifa zinazogusa maisha ya wananchi wengi wanaohitaji matibabu hayo,” alisema.
Aidha, alisema mkutano huo umefanyika kama sehemu ya kuendelea kutafuta njia za kufanikisha upatikanaji wa matibabu muhimu nchini, huku akisisitiza umuhimu wa wadau kuongeza ushiriki wao ili kusaidia kukabiliana na changamoto za gharama kubwa za huduma hizo.
Alitoa wito kwa wananchi, taasisi na wadau mbalimbali kuendelea kuunga mkono juhudi hizo za BMH ili kuwezesha wagonjwa wanaohitaji huduma za upandikizaji viungo na matibabu mengine maalumu kupata huduma kwa wakati.
Kwa mujibu wa Sillo, endapo michango itaongezeka na kufikia viwango vikubwa zaidi, hatua hiyo itasaidia kuongeza uwezo wa utoaji huduma pamoja na kuboresha miundombinu ya matibabu.
Alisema kutegemea bajeti ya serikali pekee hakuwezi kukidhi mahitaji yote yanayoongezeka ya huduma za kibingwa, hivyo ushirikishwaji wa wadau ni njia muhimu ya kuimarisha sekta ya afya na kuokoa maisha ya Watanzania wengi.

