Wizara ya Ujenzi imetangaza mpango wa kuendelea kutekeleza miradi mikubwa ya miundombinu ya barabara na madaraja katika mwaka wa fedha 2026/2027, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kupunguza msongamano wa magari katika majiji makubwa nchini na kuboresha mfumo wa usafiri mijini.
Akizungumza bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo leo Jumatano tarehe 20 Mei, 2026 , Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema serikali imejipanga kuendeleza miradi katika majiji ya Dar es Salaam, Dodoma, Arusha, Mwanza, Mbeya pamoja na miji ya Pwani, Iringa na Singida, kwa lengo la kuongeza ufanisi wa usafiri, kuchochea shughuli za kiuchumi na kuboresha maisha ya wananchi.

Katika Jiji la Dar es Salaam, serikali itaendelea na ujenzi wa awamu mbalimbali za Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT), ambapo Awamu ya Tatu inahusisha njia ya Maktaba hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kupitia Gongolamboto yenye urefu wa kilomita 23.3. Awamu ya Nne itahusisha njia ya Maktaba–Morocco–Mwenge–Tegeta pamoja na Mwenge–Ubungo yenye jumla ya kilomita 30.1.
Aidha, maandalizi ya Awamu ya Tano ya BRT kutoka Ubungo hadi Bandarini kupitia Tabata–Segerea na Tabata–Kigogo yenye urefu wa kilomita 27.6 yanaendelea, sambamba na ujenzi wa daraja la kupitisha magari (flyover) eneo la Tabata.
Serikali pia inaendelea na mipango ya ujenzi wa flyovers mbili katika maeneo ya Mwenge na Morocco, ambapo mazungumzo ya ufadhili na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) yanaendelea.
Miradi mingine ni pamoja na upanuzi wa barabara ya Ubungo–Kimara kutoka njia sita hadi nane, upanuzi wa Mbagala–Kongowe–Mkuranga pamoja na Daraja la Mzinga, upanuzi wa Barabara ya Mwai Kibaki, upanuzi wa Kibaha–TAMCO kutoka njia mbili hadi nane, pamoja na ujenzi wa flyovers katika maeneo ya Fire, Magomeni na KAMATA.Katika Jiji la Dodoma, serikali inaendelea kukamilisha ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje yenye urefu wa kilomita 112.3, ambayo iko katika hatua za mwisho. Pia kuna upanuzi wa Barabara ya Dodoma–Morogoro, ambapo sehemu ya Kimbinyiko–Chamwino itapanuliwa kutoka njia mbili hadi sita kufuatia mkataba uliosainiwa Mei 18, 2026.
Vilevile, upanuzi wa barabara za Dodoma–Iringa na Dodoma–Arusha unaendelea katika hatua za maandalizi, pamoja na ujenzi wa barabara ya mzunguko wa ndani ya jiji la Dodoma yenye urefu wa kilomita 6.4, ambayo inafadhiliwa na Serikali ya Japan kupitia washirika wa maendeleo.
Kwa upande wa Jiji la Arusha, miradi inayotekelezwa ni pamoja na upanuzi wa Barabara ya Arusha–Kisongo kutoka njia mbili hadi nne, ujenzi wa Barabara ya Mbauda–Losinyai unaoendelea, upanuzi wa Tengeru–USA River, pamoja na maandalizi ya mwisho ya ujenzi wa Barabara ya Tengeru–Mererani.
Katika Jiji la Mwanza, serikali inaendelea na taratibu za kumpata mkandarasi kwa ajili ya upanuzi wa Barabara ya Mwanza–Usagara kutoka njia mbili hadi nne, pamoja na maandalizi ya kuanza ujenzi wa Barabara ya Uwanja wa Ndege wa Mwanza–Kayenze.
Kwa upande wa mikoa ya Mbeya, Iringa, Songwe na Singida, miradi mbalimbali ya upanuzi na ujenzi wa barabara inaendelea, ikiwemo Nsalaga–Uyole–Ifisi, maandalizi ya Barabara ya mchepuo Uyole–Songwe, mradi wa PPP wa Igawa–Tunduma, ujenzi wa mchepuo wa Iringa, pamoja na maandalizi ya upanuzi wa barabara za ndani ya Mji wa Singida.
Wizara imesisitiza kuwa miradi hiyo ni sehemu ya mkakati wa taifa wa kuboresha mtandao wa usafiri mijini na kuondoa changamoto za msongamano wa magari unaoongezeka kutokana na kasi ya ukuaji wa miji nchini.
