Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanikiwa kujenga kilometa 1,495.45 za barabara kwa kiwango cha lami pamoja na madaraja makubwa 18 ndani ya kipindi cha miaka mitano, hatua iliyoelezwa kuwa mafanikio makubwa katika sekta ya miundombinu nchini.

 

Mafanikio hayo yameelezwa leo Jumatano Mei 20, 2026 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

 

Waziri Ulega amesema mtandao wa barabara za kitaifa unaosimamiwa na Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) umefikia kilometa 37,734.41, ambapo kati ya hizo kilometa 12,225.26 zimejengwa kwa kiwango cha lami.

 

Amesema wakati Tanzania inapata uhuru mwaka 1961, mtandao wa barabara za lami ulikuwa na urefu wa kilometa 1,360 pekee, huku Serikali kuanzia Awamu ya Kwanza hadi ya Tano zikijenga jumla ya kilometa 9,369.81 za barabara za lami.

 

Kwa mujibu wa Waziri huyo, kasi ya utekelezaji wa miradi ya miundombinu imeendelea kuimarika katika Serikali ya Awamu ya Sita kupitia ujenzi wa barabara na madaraja makubwa yanayorahisisha usafiri na kuchochea ukuaji wa uchumi.

 

Aidha, amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026 Wizara ilipanga kujenga na kukarabati barabara kuu na za mikoa zenye urefu wa kilometa 450 kwa kiwango cha lami pamoja na kilometa 820 kwa kiwango cha changarawe.

 

Hadi kufikia Aprili 2026, Wizara imekamilisha ujenzi na ukarabati wa kilometa 243.13 za barabara kwa kiwango cha lami na kilometa 94.36 kwa kiwango cha changarawe.

 

Katika upande wa madaraja, Waziri Ulega amesema Serikali imekamilisha ujenzi wa madaraja tisa ambayo ni Mitomoni (Ruvuma), Mirumba (Katavi), Nzali (Dodoma), Doma, Chakwale na Nguyami (Morogoro), Mkili (Ruvuma), Kalebe (Kagera) pamoja na Itembe (Simiyu), huku ujenzi wa madaraja mengine 11 ukiendelea.

Amesema Serikali pia inaendelea na maandalizi ya ujenzi wa madaraja 13 pamoja na kazi za upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa baadhi ya miradi ya madaraja katika maeneo mbalimbali nchini.