DODOMA
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela imefanya ziara katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa lengo la kujifunza namna ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya maendeleo ili kuboresha ukusanyaji wa mapato, kuinua uchumi na kuboresha upatikanaji wa huduma kwa jamii.
Ziara hiyo ilihusisha madiwani pamoja na wataalamu kutoka Manispaa ya Ilemela waliotembelea miradi mbalimbali kwa ajili ya kujifunza mbinu za usimamizi na utekelezaji.
Akizungumza kuhusu miradi hiyo, Mchumi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mataso Ndege, alisema kuwa lengo la utekelezaji wa miradi hiyo ni kuongeza mapato ya halmashauri, kupunguza utegemezi kwa serikali kuu, kuvutia uwekezaji, kupendezesha jiji pamoja na kuongeza ajira na huduma kwa wananchi.
“Utekelezaji wa miradi ya kimkakati umegawanyika katika awamu tatu ambapo awamu ya kwanza imehusisha ujenzi wa Government City Complex (Mtumba Complex), Dodoma City Hotel pamoja na Soko la wazi la Machinga, ambayo yote imekamilika. Awamu ya pili itahusisha miradi ya Nyerere Square Plaza na Nunge Investment Building, huku awamu ya tatu ikijumuisha Dodoma City Complex Mall, Dodoma City Complex Apartment na NK Complex” alisema Ndege.
Nae, Mtakwimu kutoka Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Nora Mulambo ya alisema kuwa mradi wa Dodoma City Hotel uligharimu shilingi bilioni 11.9, huku mradi wa Mtumba Complex unaojumuisha ukumbi wa mikutano unaotekelezwa kwa awamu tatu nao utagharimu jumla ya shilingi bilioni 59. Alifafanua kuwa awamu ya kwanza ya mradi huo iligharimu shilingi bilioni 18 na mradi umekamilika kwa asilimia 99. Aidha, alisema kuwa ujenzi wa Soko la wazi la Machinga uligharimu shilingi bilioni 9.5 na manufaa ya miradi hiyo yanaonekana kutokana na makusanyo ya mapato.
Kwa upande wake, Naibu Meya wa Manispaa ya Ilemela, Kuruthum Abdallah alisema kuwa ziara hiyo imelenga kupata uzoefu na mbinu zinazotumiwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika kusimamia miradi ya maendeleo. “Tumekuja kujifunza na kubadilishana uzoefu ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na utoaji wa huduma bora kwa wananchi” alisema Abdallah.
Ziara hiyo inatarajiwa kuimarisha ushirikiano kati ya halmashauri hizo mbili pamoja na kuongeza uwezo wa kiutendaji katika kusimamia na kutekeleza miradi ya maendeleo yenye tija kwa wananchi.

