Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali itaendelea kuimarisha mfumo wa stakabadhi ghalani ili kuongeza tija kwa wakulima, kuimarisha masoko ya mazao pamoja na kukuza uchumi wa viwanda nchini. Ameyasema hayo leo Mei 19, 2026 jijini Dodoma wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 20 ya Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi Ghala

Amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameendelea kuwa mstari wa mbele katika kulinda bidhaa za viwandani na kuimarisha sekta ya uzalishaji kupitia ongezeko la bajeti pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa masoko ya bidhaa mbalimbali.

Aidha, Waziri Mkuu amewataka Watanzania kuunga mkono mageuzi ya kiuchumi yanayoendelea nchini huku wakishiriki kutatua changamoto zinazojitokeza katika sekta ya uzalishaji na biashara.

Amesema wananchi wanaotumia mfumo wa stakabadhi za ghala wamekuwa wakinufaika zaidi tofauti na wale wanaouza mazao yao kiholela, kwani mfumo huo umeongeza ubora wa bidhaa, ushindani wa soko pamoja na kuongeza fursa za masoko ya uhakika.

Dkt. Mwigulu amesema Serikali itaendelea kushughulikia changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo ikiwemo umbali wa maghala kutoka maeneo ya uzalishaji wa mazao.

Katika hatua nyingine, ameielekeza Bodi ya Stakabadhi za Ghala kufanya kikao maalumu kabla ya bajeti kuu ya Serikali kusomwa ili kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa maghala mapya nchini.

Pia amezitaka taasisi za fedha kuweka mfumo wa malipo ya awali kwa wakulima ili kuondoa changamoto ya kucheleweshewa malipo ya mazao yao.

Aidha amesema Serikali inaendelea kufanya mageuzi katika mfumo wa dhamana kwa kuruhusu matumizi ya mali nyingine pamoja na nyaraka mbalimbali ikiwemo vyeti vya elimu ili kuwawezesha wananchi kupata mikopo kwa urahisi.

Kwa upande wake Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga amesema mafanikio ya miaka 20 ya mfumo wa stakabadhi ghalani yametokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali pamoja na jitihada za kutafuta masoko ya uhakika kwa mazao ya wakulima.

Kwa Upande wake  Mwenyekiti wa Bodi ya Stakabadhi za  Ghala, Bi. Geraldine Rashel amesema mfumo huo umeendelea kuimarisha upatikanaji wa mikopo kwa wakulima na kuongeza imani kwa wadau wa ushirika katika kipindi cha miaka 20 iliyopita.

Awali akizungumza, Mkurugenzi Mtendaji wa WRRB, Bw. Asangye Bangu amesema wadau wa mfumo wa stakabadhi ghalani wamefikia maazimio mbalimbali ikiwemo kutambuliwa rasmi kwa wadau wa sekta hiyo ili kuongeza ufanisi wa mfumo huo nchini.