📍Bungeni Dodoma

MBUNGE wa Jimbo la Same Mashariki mkoani Kilimanjaro, Anna Kilango Malecela ameendelea na jitihada zake za kuhakikisha wananchi wa jimbo hilo wanapata huduma za afya karibu zaidi ambapo leo Bungeni amehoji ujenzi wa kituo cha Afya katika kata ya Kalemawe.

Akiuliza swali hilo, Anna Kilango alisema kuwa, kata ya Kalemawe ni kata ambayo ipo pembezoni na imesimama yenyewe sehemu ya ziwani na wakati wa kampeni kata hii iliahidiwa kujengewa kituo cha Afya na Mkurugenzi wa wilaya ya Same alilisimamia hili je serikali mnasemaji kuhusu ujenzi wa kituo cha afya kata ya Kalemawe.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Tamisemi alisema kuwa, ni dhamira ya serikali kusogenza huduma za afya karibu na wananchi hususani vituo vya afya ili kupata huduma za dharura za upasuaji kwa kinamama wajawazito na wananchi wengine.

Alisema kuwa, katika eneo hilo swala la muhimu ni kufanya tathimini ya vigezo ikiwemo idadi ya wananchi katika kata usika na umbali wa kutoka kituo cha jirani kinachotoa huduma za upasuaji na upatikanaji wa eneo linalotosheleza mahitaji ya kituo cha afya na kumwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Same kuwasilisha taarifa na kuchanganua ikiwa vigezo vinafikiwa ili Ofisi ya Waziri Mkuu Tamisemi ianze kutenga bajeti ya kuanza ujenzi wa kituo hicho endapo vigezo vitafikiwa.