Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi, Elbariki Kingu amesema kuwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania linaendelea kuonesha utulivu, nidhamu na uzalendo wa hali ya juu katika kulinda amani na usalama wa taifa.
Kingu ametoa kauli hiyo Bungeni jijini Dodoma leo Jumanne Mei 19, 2026 wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Amesema uongozi wa sekta ya ulinzi chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu Hassan umechangia kwa kiasi kikubwa kuimarika kwa nidhamu na mshikamano ndani ya vyombo vya ulinzi na usalama.
Aidha, Kingu amesisitiza kuwa moja ya mambo anayoyathamini zaidi katika uongozi ni unyenyekevu, akieleza kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Rhimo Nyansaho ameendelea kuonesha unyenyekevu, busara na ushirikiano wa karibu katika kusimamia wizara hiyo, jambo linalochangia ufanisi na utulivu wa sekta ya ulinzi.
Amesema Jeshi la Wananchi wa Tanzania limeendelea kuwa mfano wa kuigwa katika kulinda Katiba, mipaka na tunu za taifa, akibainisha kuwa hali hiyo imeongeza imani ya wananchi kwa jeshi hilo.
Ameongeza kuwa katika nyakati mbalimbali za changamoto, jeshi hilo lilibaki imara kwa kutekeleza majukumu yake kwa weledi na uadilifu, hali inayodhihirisha uzalendo wake kwa taifa.
Pia amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha sekta ya ulinzi ili iweze kukabiliana na changamoto za kiusalama na kudumisha amani ya nchi.
Katika hotuba yake, ametoa pongezi kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jacob Mkunda kwa uongozi wake katika kusimamia nidhamu na utendaji wa jeshi hilo.
