WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni Serikali inayowajibika kwa wananchi na ipo tayari kuyafanyia kazi maoni yote yaliyotolewa na Wabunge kuhusu Sekta ya Maliasili na Utalii.

Waziri Mkuu amesema hayo leo Jumatatu (Mei 18, 2026) wakati akitoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja zilizotolewa na Wabunge katika mjadala wa kupitisha Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Bungeni jijini Dodoma 

Amesema tayari Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelekeza Wizara ya Maliasili na Utalii kushirikiana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Wizara ya Katiba na Sheria kupitia upya masuala mbalimbali yanayohusu sekta hiyo, ikiwemo sheria namba 111 na 116.

“Hoja zote zilizotolewa na Wabunge tumezipokea na tutazifanyia kazi. Pamoja na mambo mengine, tutaenda kuangalia upya masuala yanayohusiana na mipaka hasa baadhi ya maeneo ambayo mipaka haijulikani ni ipi, ili wananchi wajue mipaka katika maeneo yao,” amesema Dkt. Mwigulu.

Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali imebaini kuwepo kwa changamoto katika baadhi ya sheria za uhifadhi, hususan zinazohusiana na utoaji wa adhabu ambazo kwa sasa zinafanana hata kwa makosa yenye uzito tofauti.

Amesema katika hali ya sasa, sheria zinaweka adhabu zinazofanana kwa makosa tofauti ikiwemo mtu anayekutwa na mkaa na anayehusika na biashara haramu ya meno ya tembo, pamoja na mkulima anayelima ndani ya maeneo ya hifadhi na mtu anayejihusisha na ujangili.“Sheria zetu ambazo zilikuwepo kwenye haya masuala ya hifadhi, adhabu zake zinaendana. Mwenye mkaa na aliyebeba meno ya tembo wote wanapata adhabu inayofanana. Yule aliyelima mazao yake na yule anayefanya ujangili, zote zinafanana,” amesema.

Dkt. Mwigulu amesema kutokana na maelekezo ya Rais Samia, Serikali itaangalia upya sheria hizo kwa lengo la kuhakikisha zinaboresha ustawi wa wananchi ili kuwa na uhifadhi na utalii endelevu kwa manufaa ya taifa.