Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Ellen Maduhu, tarehe 18 Mei 2026 amekutana na kuzungumza na Balozi Mkazi wa Jamhuri ya Serbia nchini, Mhe. Jovica Topalović, katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kuendelea kuimarisha uhusiano wa muda mrefu uliopo kati ya Tanzania na Serbia.
Katika mazungumzo hayo, Balozi Topalović amewasilisha ujumbe maalum kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Serbia, Mhe. Aleksandar Vučić, uliomualika Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kufanya ziara rasmi nchini Serbia.
Vilevile, pande hizo mbili zimejadili maandalizi ya ziara hiyo inayotarajiwa kufanyika hivi karibuni, huku zikisisitiza dhamira ya pamoja ya kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali za kimkakati, ikiwemo biashara, uwekezaji, utalii, kilimo, afya, elimu pamoja na teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA).

