Dodoma, Jumatatu, Mei 18, 2026

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na Benki Kuu ya Tanzania (BOT), zimezindua rasmi utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano yatakayowezesha utoaji wa elimu ya fedha kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu nchini baada ya taasisi hizo mbili za umma kusaini hati za makubaliano ya ushirikiano (MoU).

Uzinduzi huo umefanyika leo Jumatatu, Mei 18, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya BOT jijini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi kutoka HESLB na BOT pamoja na wadau mbalimbali wa sekta za elimu na fedha.

Akizungumza katika hafla hiyo, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba ameipongeza HESLB kwa kuendelea kubuni na kuimarisha programu zinazolenga kuwawezesha wanafunzi kupata stadi za kifedha zitakazowasaidia kusimamia fedha zao kwa ufanisi wakiwa vyuoni na hata baada ya kuhitimu masomo yao. 

“Ninaipongeza HESLB kwa kutambua umuhimu wa elimu ya fedha kwa wanafunzi na kwa kushirikiana na BoT katika utekelezaji wa mpango huu muhimu. Vilevile, ninathamini juhudi zilizofanywa na timu za wataalam kutoka taasisi zote mbili katika kuandaa Hati hii ya Makubaliano (MoU)”, amesisitiza Gavana Tutuba.

Kupitia ushirikiano huo, kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, wanafunzi wanaonufaika na mikopo ya elimu ya juu watanufaika na programu maalum ya elimu ya fedha kupitia mfumo wa akaunti binafsi za wanafunzi unaojulikana kama Student’s Individual Permanent Account (SIPA).

Programu hiyo itatoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya fedha, uandaaji wa bajeti, uwekaji wa akiba, matumizi yenye tija ya mikopo, huduma za fedha kidijitali pamoja na ulinzi wa mtumiaji wa huduma za kifedha. 

Dkt. Kiwia amesema hatua hiyo inalenga kujenga kizazi cha vijana wenye uelewa wa kifedha, uwajibikaji na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi ya kifedha kwa maendeleo yao binafsi na taifa kwa ujumla.

“Kupitia elimu hii ya fedha, ni matumaini yetu makubwa kuwa wanafunzi watajenga nidhamu ya matumizi ya fedha, kujiwekea mipango ya kifedha, kuelewa umuhimu wa kuweka akiba, pamoja na kutimiza wajibu wao wa kurejesha mikopo kwa wakati. Hii itasaidia kuongeza uendelevu na ustahimilivu wa mfuko wa mikopo ya wanafunzi na kuwezesha wanafunzi wengi zaidi kunufaika katika miaka ijayo”, amesema Dkt. Kiwia.

Aidha, programu hiyo itapatikana kupitia majukwaa ya kidijitali ili kuwawezesha wanafunzi kote nchini kupata elimu hiyo kwa urahisi bila kujali eneo walipo.

Katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB pia amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wadau mbalimbali wakiwemo wazazi, walezi, taasisi za fedha na watoa huduma za mawasiliano katika kuhakikisha elimu hiyo inawafikia wanafunzi wengi zaidi.

Uzinduzi wa utekelezaji wa makubaliano hayo unaenda sambamba na juhudi za Serikali za kuimarisha huduma jumuishi za kifedha na kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya uchumi wa nchi.