Na John Mapepele, Geneva, Uswisi
Waziri wa Afya Nchini, Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa ameongoza ujumbe wa Serikali ya Tanzania katika ufunguzi rasmi wa Mkutano Mkuu wa 79 wa Shirika la Afya Duniani (WHA79) ulioanza leo Mei 18, 2026 mjini Geneva, Uswisi.
Mkutano huo mkubwa duniani katika sekta ya afya unashirikisha zaidi ya nchi 180 katika maeneo mbalimbali ulimwengu umefunguliwa na
Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).
“Mkutano wa 79 wa Baraza la Afya Duniani (WHA79) unafanyika kuanzia tarehe 18 hadi 23 Mei 2026 mjini Geneva, Uswisi. Mkutano huu unawakutanisha wajumbe kutoka Nchi Wanachama wa WHO ili kushughulikia shinikizo kubwa linaloikabili mifumo ya afya na kuweka sera za afya za kimataifa, huku ukisisitiza sana huduma ya afya kwa wote, afya ya akili, na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa afya.” Amefafanua Mheshimiwa Mchengerwa
Kwa mujibu wa Mheshimiwa Mchengerwa, maeneo makuu ya mjadala katika mkutano wa mwaka 2026 ni pamoja na:
Huduma ya Afya kwa Wote (UHC) na Ufadhili ambapo amesema Nchi wanachama na mashirika ya kiraia wanatoa kipaumbele kwa kuharakisha mifumo ya ufadhili wa afya inayoongozwa na nchi husika, mageuzi ya kidijitali katika mifumo ya afya, na kuhakikisha ushiriki wa kijamii ili kuimarisha mamlaka ya afya ya kitaifa.
Aidha amesisitiza eneo jingine linalopewa mkazo ni Afya ya Akili ambapo amesema kufuatia Mkutano wa Ngazi ya Juu wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 2025 kuhusu Magonjwa Yasiyoambukiza (NCDs) na afya ya akili, WHA79 ina kampeni kubwa za utetezi na matukio maalum yanayolenga kutafsiri ahadi za kimataifa kuwa mikakati halisi ya kitaifa ya afya ya akili.
Jambo jingine litakalojadiliwa ni Tabianchi na Afya ambapo amefafanua kuwa ingawa si ajenda maalum ya pekee, athari zinazoendelea za mzozo wa tabianchi na matumizi ya mafuta ya kisukuku ni sehemu muhimu ya mijadala inayohusu afya ya uzazi, magonjwa yasiyoambukiza, na usimamizi wa magonjwa.
Amesem WHO pia inazindua mpango wa kimataifa wa utetezi uliokusudiwa kudumisha msukumo kuelekea mkutano ujao wa COP31 kuhusu tabianchi.
Mkakati wa Kimataifa na Uongozi: Wajumbe wanajadili namna ya kuoanisha mageuzi mbalimbali ya afya ya kimataifa ili kuhakikisha matokeo yenye usawa na uwajibikaji.
Aidha, mkutano huu unaweka msingi wa uchaguzi ujao wa Mkurugenzi Mkuu wa WHO, huku wagombea wakianza kutangazwa rasmi na kundi jipya la nchi likichaguliwa kuingia katika Bodi ya Utendaji.
Pia ameongeza kwamba mkutano huu pia utajadili taarifa na Mikakati ya Magonjwa ambapo ajenda ya muda ya mkutano inajumuisha hatua zinazoendelea kwa mpango wa kutokomeza malaria, Ajenda ya Chanjo 2030, na mkakati wa kumaliza ugonjwa wa kifua kikuu (TB).
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huu ulioongozwa na Mheshimiwa Mchengerwa umeshirikisha Mheshimiwa Balozi Abdala Possi, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa na Mashirika Mengine ya Kimataifa Mjini Geneva, Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Afya na Ukimwi, Mheshimiwa, Dkt. Johannes Lukumay, Katibu Mkuu Dkt. Seif Shekalaghe, Mganga Mkuu wa Serikali
, Dkt. Grace Magembe na baadhi ya watendaji wa Wizara ya Afya.
Tanzania inatarajia kuwasilisha mawasilisho kadhaa katika mkutano huo na kufanya majadiliano na wadau mbalimbali wa afya pembezoni mwa mkutano huo.WAZIRI MCHENGERWA AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA WHA79.

