Ruvuma

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umetoa elimu kwa zaidi ya vijana 300 wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma kuhusu fursa mbalimbali za kiuchumi zinazopatikana kupitia sekta ya misitu, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuwawezesha vijana kujikwamua kiuchumi.

Elimu hiyo ilitolewa katika jukwaa la vijana lililofunguliwa rasmi na Mkuu wa Wilaya ya Songea, Mhe. Kapenjama Ndile, ambaye aliwataka vijana kuzingatia maadili mema, nidhamu na uwajibikaji ili waweze kutumia ipasavyo fursa zinazotolewa na Serikali pamoja na taasisi mbalimbali.

Akizungumza katika jukwaa hilo Jumamosi Mei 16, 2026, Mhe. Ndile alisema mafanikio ya vijana yanategemea juhudi binafsi, kujituma na uaminifu katika kazi wanazozifanya.

“Changamoto kubwa kwa vijana wengi si ukosefu wa fursa, bali ni ukosefu wa nidhamu na uwajibikaji katika kuzitumia fursa hizo,” alisema Ndile.

Katika mada iliyowasilishwa na Mhifadhi Daraja la Kwanza (CR I), Daud Mandingo, kwa niaba ya Mhifadhi Mkuu wa TFS Shamba la Miti Wino, vijana hao walipatiwa elimu kuhusu fursa mbalimbali zinazotokana na shughuli za misitu.

Fursa hizo ni pamoja na ajira za msimu katika Shamba la Miti Wino, hususan shughuli za palizi, upandaji na utunzaji wa mashamba ya miti.

Aidha, Mandingo alieleza kuwa TFS pia inatoa fursa kupitia ufugaji wa nyuki, ugawaji wa miche ya miti, elimu ya upandaji na uhifadhi wa misitu pamoja na ugawaji wa mizinga kwa vikundi vya vijana ili kuwawezesha kujiajiri na kuongeza kipato.

Baadhi ya vijana walioshiriki jukwaa hilo walisema elimu waliyoipata imewasaidia kutambua fursa zilizopo katika sekta ya misitu na kuwaongezea hamasa ya kushiriki katika shughuli za uzalishaji pamoja na uhifadhi wa mazingira.