
Akizungumza katika Full Shangwe ofisini kwake leo Iringa Mjini, Kikoti alisema kuwa kizazi cha sasa kina nafasi kubwa katika ujenzi wa Tanzania, lakini nafasi hiyo haiwezi kutumika ipasavyo bila misingi imara ya maadili na kujituma kwenye shughuli za kila siku.
Aliongeza kuwa vijana wengi wamekuwa wakipoteza muda kwenye mambo yasiyowasaidia, jambo linalowakosesha ufanisi na nafasi za kujikwamua kiuchumi.
Katika maelezo yake, mwenyekiti huyo aliwahimiza vijana kupanua upeo wa fikra na kujihusisha zaidi na shughuli za kiuchumi kama kilimo, biashara, ufugaji, ujasiriamali, teknolojia, michezo na sanaa.
Aidha, Kikoti alionya juu ya mwenendo unaokwamisha vijana wengi, ikiwemo matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, kutojiwekea malengo, pamoja na kutegemea mafanikio ya haraka bila kufanya kazi kwa bidii.Alisema kuwa uchumi wa sasa unahitaji vijana wanaoweza kushindana kimaarifa na kwa kasi, jambo litakalowezekana tu endapo vijana watawekeza katika uwezo wao binafsi.
Katika wito kwa jamii, alitaka wazazi, walezi na viongozi wa maeneo mbalimbali kushirikiana katika kujenga nidhamu na uwajibikaji kwa vijana, akibainisha kuwa vijana ni nguvu ya taifa na wanahitaji kuongozwa kwa njia sahihi ili kufikia malengo yao.
Kwa upande wa chama, aliwataka viongozi wa UVCCM kuandaa programu endelevu zitakazowaimarisha vijana kielimu, kiuchumi na kimaadili, kwa kuwa chama kina jukumu la kulea kizazi kitakachoweza kuongoza nchi katika miaka ijayo.
Kikoti alihitimisha kwa kuwataka vijana kuona uwajibikaji kama silaha ya mafanikio na msingi wa kujijengea heshima katika jamii.
Alisema kuwa safari ya mafanikio inaanza na maamuzi madogo yanayofanywa kila siku, na kwamba kila kijana anapaswa kujiuliza anachokifanya leo kitamweka wapi miaka michache ijayo.
